Mfahamu Mkimbizi aliyeshinda tuzo kwa kuandika kitabu kupitia whatsApp - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Saturday, February 2, 2019

Mfahamu Mkimbizi aliyeshinda tuzo kwa kuandika kitabu kupitia whatsApp

Mkimbizi na mwanahabari aliyezuiliwa kwa miaka kadhaa katika gereza la kisiwa cha bahari ya Pacific, ameshinda tuzo ya fasihi Australia. Behrouz Boochani, raia wa Iran, aliandika kitabu kwa jina- No Friend But the Mountains: yaani ”Hakuna marafiki lakini milima” – Utunzi kutoka gereza la Manus.Kwa mujibu wa BBC, Boochani, alitumia mtandao wa kijamii wa WhatsApp kuandika kitabu hicho akiwa gerezani.
Boochani ambaye bado anazuiliwa katika gereza la Manus, eneo la Papua New Guinea hajaruhusiwa kuingia nchini Australia kupokea zawadi ya dola 100,000 (£55,000).
Gereza hilo tata lilifungwa mwaka 2017 lakini yeye na mamia ya watu wengine walihamishiwa vituo vingine mbadala.
Akizungumza na BBC kutoka kisiwa cha Manus, usiku ambao waandishi wenzake walioshinda tuzo walikua wakisherehekea mjini Melbourne, Boochani alisema ushindi huo umempatia “mchanganyiko wa hisia”.


“Nasikia raha sana kwa sababu tumeweza kuangazia suala ambalo linawagusa watu wengi, bila shaka sasa ulimwengu utafahamu hali ngumu wanayopitia ,hilo ni jambo jema …lakini kwa upande mwingine sioni haja ya kufurahia kwasababu marafiki zangu wengi wanateseka mahali hapa”.
Kitabu hicho kiliandikwa kwa lugha ya Farsi kupitia ujumbe katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp, na kutumiwa mtafsiri Omid Tofighian, wakati ambapo Boochani akiwa jela.
“WhatsApp ni kama ofisi yangu,”alisema. “Sikuandika kwa karatasi kwasababu wakati huo walinzi walikua wakifanya upekuzi katika chumba chetu kila wiki au mwezi. Nilikua na hofu ya kupoteza kazi yangu, kwa hivyo ilikuwa bora kwangu kuandika na kumtumia mfasiri wangu.”
Boochani, alizuiliwa mara ya kwanza mwaka 2013 baada ya kuingia nchini humo kwa boti kutoka kusini mashariki mwa Asia.
Australia ina sera kali dhidi ya wakimbizi wanaowasili chini humo kwa boti kutafuta hifadhi, na imeapa kuwa haitawapatia hifadhi wakimbizi kama hao kwasababu wanahatarisha maisha yao kuingia nchini humo
Mwaka jana, Marekani ilikubali kuwapatia hifadhi wakimbizi waliokuwa wakizuiliwa katika jela ya Manus na taifa la kisiwani la Nauru.


Zaidi ya wakimbizi 100 wameondolewa lakini Boochani anasubiri taarifa kutoka kwa maafisa wa Marekani baada ya kufanya mahojiano miezi kadhaa iliyopita.
Amepewa hadhi ya ukimbizi na Papua New Guinea lakini sawa na wakimbizi wengine hataki kuishi huko.
Amesema aliamua kutoroka Iran kufuatia mvutano wa kazi yake ya uandishi na mamlaka ya nchi hiyo: “Nilihofia kufungwa jela nchini Iran kwa hivyo nikaamua kukimbilia Australia na kwa bahati mbaya nilipofika wakanikamata na kunifungia kwa miaka kadhaa.”
Waamuzi wa tuzo hiyo walielezea kitabu chake kama “kazi ya ajabu ya sanaa na nadharia muhimu ambayo inaibua hisia kwa njia rahisi”.
Masharti ya kuingia kwa Tuzo ya fasihi ya Australia ni kwamba waandishi lazima wawe raia wa Australia au wakazi wa kudumu.


Lakini kituo cha Wheeler Centre, ambacho kinasimamia tuzo hiyo kilikubali ombi la waamuzi na kukubali kushirikisha kitabu cha Boochani katika shindano la kuwania tuzo hiyo.
Sera ya wakimbizi ya Australia imeangaziwa sana na vyombo vya habari duniani na kukosolewa na Umoja wa Mataifa makundi ya kutetea haki za binadamu lakini baadhi ya wanasiasa wa Ulaya wamezisifia sana.
Lakini Boochani anataka wasomaji wa kitabu chake kuelewa kuwa kumekuwa na njama ya kuwavua wakimbizi “Utambulisho na utu wao”.
“Sisi sio malaika wala watu wabaya,”  alisema. “Sisi ni binadamu, watu wa kawaida, hatuna ubaya wowote.”
Mwezi mmoja umepita tangu alipofungiwa katika gereza la Manus.
‘Mimi ni kipande cha nyama kilichotupwa katika eneo lisilojulikana; gereza lenye uchafu na joto kali.
Naishi kati ya mamia ya watu wenye nyuso za hasira, wengine wana hofu. Kila wiki ndege moja au mbili zinatua katika uwanja wa ndege wa kisiwa hiki na watu wengi hutolewa na kutupwa ndani ya jela letu ambapo wanachanganyika nasi kama kondoo waliyofikishwa kichinjioni’ amesema Boochani.
Loading...

No comments: