R Kelly Akamatwa Na PolisiMWANAMUZIKI wa R&B R.Kelly amekamatwa baada ya kujisalimisha polisi hapo jana usiku baada ya Mahakama ya Chicago kutoa amri ya kukamatwa kwake kufuatia ushahidi mpya kuhusiana na madai kwamba aliwanyanyasa kingono  watoto watatu wenye umri wa kati ya miaka 13 na 17.
Hakimu amechukua hatua hiyo baada mkanda wa video kuonyesha tukio lililotokea mwaka 1998.
Jana usiku Februari 22, R. Kelly alielekea kwenye kituo cha polisi jijini Chicago majira ya saa 2:15 usiku baada ya kutolewa kwa maagizo ya kukamatwa kwake kufuatia tuhuma hizo za kingono.
Msemaji wa Polisi, Anthony Guglielmi, alieleza muda mfupi baadaye kuwa Kelly amekamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumamosi hii.
Wakati wa tukio hilo mwanasheria wa msanii huyo, Steve Greenberg, aliviambia vyombo vya habari kuwa wanawake hao wanamzushia tu Kelly ili kujitengenezea kipato.
”Kila mwanamke kwenye documentary hii ana nyimbo, na sasa wanaenda kuziachia, vitabu ambavyo wanaenda kuviachia, hivyo ndivyo wanavyoenda kufanya kwa sasa, kila mmoja anajaribu kuona ananufaika kupitia R. Kelly,” amesema mwanasheria huyo wa R. Kelly.
Wanawake wengine wawili walijitokeza na madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mwanamuziki wa R&B,R Kelly. Rochelle Washington na Latresa Scaff walizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuwa walipewa kinywaji pamoja na madawa ya kulevya mara baada ya tamasha la mwanamuziki huyo lililofanyika Baltimore miaka ya 1990.
Kelly mwenye umri wa miaka 52, amekuwa akishutumiwa kwa madai ya unyanyasaji wa kingono kwa wanawake kwa miongo kadhaa lakini hakuwahi kukamatwa wala kukiri makosa yake.

Post a Comment

0 Comments