SIKU 7 BAADA YA KUOANA… NDUGU WACHARUKA NDOA YA KINYAIYA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, February 26, 2019

SIKU 7 BAADA YA KUOANA… NDUGU WACHARUKA NDOA YA KINYAIYAMAMBO ni mengi tatizo ni muda! Siku saba baada ya kufunga ndoa na kuibua mjadala mzito, mtangazaji na mwigizaji maarufu Bongo, Ben Kinyaiya ameendelea kuzua gumzo, safari hii ndugu wa upande wa mke wamecharuka vibaya mno, Risasi Jumamosi limedokezwa.  
Baada ya kuzuka kwa maneno mengi ya hapa na pale hasa kwenye mitandao ya kijamii kuwa jamaa huyo ameoa mtu mzima, Ben ambaye ni mtangazaji wa Channel Ten na mwigizaji wa Tamthiliya ya Huba amejikuta akicharukiwa na ndugu wa mwanamke kwa kushindwa kumtetea ubavu wake huyo.
TUJIUNGE NA NDUGU 
Kwa mujibu wa mmoja wa ndugu wa mwanamke aliyefunga ndoa na Ben aliyezungumza na gazeti hili kwa niaba ya ndugu wengine, wamechukizwa ile mbaya na kitendo cha Ben kulikalia kimya suala hilo huku kukiwa na mjadala kila kona. Alisema kibaya zaidi kwenye huo mjadala, ndugu yao amekuwa akitukanwa na kuambiwa maneno mengi ya shombo, lakini Ben amekuwa hataki kujitokeza na kueleza ukweli wa ndoa yao.
KWA NINI ASIJITOKEZE? 
Ndugu huyo alifunguka kwamba, anaamini kuwa kama Ben angetaka ndugu yao asitukanwe kwenye mitandao ya kijamii kila kukicha, basi angejitokeza na kuanika ukweli kuhusiana na kile kinachosemwa juu ya ndugu yao.
“Yaani mkeo kabisa anasimangwa kila kukicha kwenye mitandao ya kijamii halafu unanyamaza? “Kama kweli mtu una mapenzi ya dhati kwake, kwa nini ufichefiche? “Kwa nini asiweke kila kitu wazi maana angeweka wazi, watu wangeheshimu uamuzi wake maana inavyoonekana ni kama anataka kujifanya siyo kweli bali ni filamu,” alisema ndugu huyo kwa sharti la kutotajwa gazetini.
NI KWELI BEN AMEOA 
Ndugu huyo alisisitiza kuwa ni kweli Ben amemuoa mchumba wake huyo wa siku nyingi. “Ndoa ilifungwa pale kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala (Boma) jijini Dar hivyo siyo kitu cha kusema kwamba ni filamu bali ni jambo linalotambulika kiserikali. “Ukweli ni kwamba Ben alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na ndugu yetu kwa takriban miaka miwili sasa.

“Cha msingi yeye atuambie kama hakumpenda ili tujue kabisa maana wanaume wa siku hizi ni shida sana. Inawezekana amemuona ndugu yetu yupo kwenye maisha mazuri, akatamani maisha zaidi kuliko mapenzi,” alifunguka kwa jazba ndugu huyo akisisitiza kwamba wanachukizwa na kitendo cha Ben kufichaficha suala hilo.
HUYU HAPA BEN 
Kutokana na kucharuka kwa ndugu hao, gazeti hili lilimtafuta Ben ambapo bila nukta wala koma, aliwachana ‘live’ wale ambao wako bize mitandaoni kuisema ndoa yake ambayo amefunga hivi karibuni na mwanamama huyo aliyekuwa akiishi nchini Uingereza. Ben alisema kuwa wale ambao wanamfuatilia na kusema kuwa huenda kuna kitu ambacho amekifuata kwa mwanamke huyo wamuache kwani huo ni uamuzi wake binafsi na wala hakulazimishwa na mtu.
“Wale ambao wananisema kuhusu ndoa yangu hayawahusu, maana wanaongea sana. “Wapo wanaosema mara nimefuata pesa, mara ni kwa sababu nataka kwenda kuishi Uingereza, mimi hayo siyaelewi kwa kuwa wao ndiyo wanayaongea. “Mimi ninasisitiza tu kuwa wanaweza kuzungumza mambo mengi, lakini ukweli ni kwamba hayawahusu,” Ben alihitimisha mjadala kisha akakata simu.
TUJIKUMBUSHE 
Ilikuwa Jumamosi iliyopita ambapo Ben alidaiwa kufunga ndoa ya kiserikali na mwanamke wake huyo ambaye anatajwa kuwa mchumba wake wa siku nyingi, baada ya picha zao kusambaa katika mitandao ya kijamii. Mara baada ya picha hizo za harusi kusambaa, mara moja maneno yaliibuka kutokana na muonekano wa bibi harusi ambapo wapo waliodai kuwa mwanamke huyo ni mtu mzima kuliko Ben ‘Shuga Mama’.
Lakini pia kuna maneno yaliyosambaa kuwa huenda harusi hiyo ilikuwa ni muvi kwani mashabiki wa Ben hawakuamini kuwa mwanamke huyo ndiye mke mtarajiwa wa staa huyo


STORI: Imelda Mtema na Neema Adrian

CHANZO; GLOBAL PUBLISHERS 

Loading...

No comments: