WAHASIBU, MAMENEJA TEMESA WAPEWA MAFUNZO YA UKUSANYAJI MADUHURI YA SERIKALI KWA KUPITIA MFUMO WA (GePG) - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Sunday, February 10, 2019

WAHASIBU, MAMENEJA TEMESA WAPEWA MAFUNZO YA UKUSANYAJI MADUHURI YA SERIKALI KWA KUPITIA MFUMO WA (GePG)


 
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akipokea muhtasari wa mafunzo ya Mfumo wa Ukusanyaji Maduhuri ya Serikali (GePG) kutoka kwa mhasibu Bi. Sophia Lukas mara baada ya kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam na kuendeshwa na wakufunzi kutoka Wizara ya Fedha na mipango (Hazina).

 
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akizungumza na wahasibu wa wakala huo kutoka mikoa mbalimbali mara baada ya kufunga mafunzo ya Mfumo wa Ukusanyaji Maduhuri ya Serikali (GePG) yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Wizara ya Fedha na mipango (Hazina). Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle katikati akizungumza na wahasibu (hawapo pichani) wakati akifunga mafunzo ya Mfumo wa Ukusanyaji Maduhuri ya Serikali (GePG) yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Wizara ya Fedha na mipango (Hazina). Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha GePG Bazil Baligumya, Mhandisi Sylvester Simfukwe, Mhandisi Lukombe King’ombe na CPA Hans Lyimo.
NA ALFRED MGWENO- TEMESA
Wahasibu na mameneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) mwishoni mwa wiki hii wamepatiwa mafunzo ya Mfumo wa Ukusanyaji Maduhuri ya Serikali, mafunzo hayo yaliyotolewa na wawezeshaji kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Hazina kitengo cha (GePG) yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mt. Depot Keko jijini Dar es Salaam na yamelenga kuwapatia uelewa mpana wa matumizi ya mfumo huo na jinsi ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kwenye utekelezaji wa mfumo huo.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle alisema mfumo huo utausaidia sana Wakala kwenye utendaji kazi wake kwani utapunguza gharama za uendeshaji kwakuwa hauna tozo lolote na wakati huo huo mtumiaji atakuwa na uwezo wa kupata taarifa wakati wowote akizihitaji.
‘’Ninaamini mfumo huu utatusaidia kutoa taarifa mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya taasisi yetu hivyo basi tuutumie kama kitendea kazi chetu muhimu katika kuboresha na kuongeza tija kwa maslahi mapana ya Wakala wetu, wizara na taifa kwa ujumla’’, alisema Mhandisi Maselle.
Naye mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Hazina kitengo cha (GePG) Ndugu Bazil Baligumya alisema mfumo huo utaisaidia TEMESA kuhakiki kwa urahisi malipo yote yatakayokuwa yanafanywa na wateja wake na utarahisisha upatikanaji wa taarifa za fedha zinazohitajika kutoka katika vituo, ‘’tumewafundisha jinsi ya kuandaa ankara za madai, kuangalia na kuhakiki malipo yaliyokwisha fanywa na wateja, namna ya kutambua na kufanya usuluhisho kwa kutumia taarifa itokayo katika mfumo wa (GePG) pamoja na taarifa ya makusanyo kutoka benki na jinsi mfumo unavyoweza kuzalisha taarifa za wateja’’, aliongeza mkufunzi huyo.
Mfumo huo wa ukusanyaji wa maduhuri ya serikali unatambua na kukusanya fedha zote za Umma na kuziweka kwenye akaunti maalumu ya serikali iliyopo Benki kuu (BOT) na umetokana na marekebisho ya sheria ya mwaka (2017 sura ya 348 kifungu cha 6 cha sheria ya fedha kifungu kidogo cha 6a i na ii) inayoelekeza fedha zote za umma kukusanywa kwa mfumo huo. Mfumo wa (GePG) ulianza kwa kutumiwa na jeshi la polisi nchini hususani askari wa barabarani pamoja na Wakala wa Misitu ambapo ulionyesha mafanikio makubwa na hivyo kupata baraka za kuenezwa zaidi katika taasisi na asasi zaidi za serikali ambapo hadi kufikia sasa wadau zaidi ya 500 wameshaunganishwa kwenye mfumo huo.
Loading...

No comments: