WANANCHI WATAKIWA KUJIUNGA NA MFUKO TAIFA WA BIMA YA AFYA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Wednesday, February 13, 2019

WANANCHI WATAKIWA KUJIUNGA NA MFUKO TAIFA WA BIMA YA AFYA


WANANCHI wametakiwa kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ili kuondokana na adha wanayoipata pale wanapopata maradhi kwa kushindwa kugharamia matibabu na kusababisha madeni , umaskini na pengine kifo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo wakati alipohudhuria mkutano wa wadau wa Bima ya Afya kwa wananchi walio katika Sekta zisizo Rasmi uliojumuisha wadau kutoka nchi mbalimbali uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar Es Salaam.

Mwenyekiti wa bodi ya Mfuko wa Taifa (NHIF) Bi. Anna Makinda akiongea mbele ya wadau wa Bima ya Afya kwa wananchi walio katika Sekta zisizo Rasmi katika mkutano uliojumuisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali uliofanyika Jijini Dar Es Salaam.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza mbele ya wadau wa Bima ya Afya kwa wananchi walio katika Sekta zisizo Rasmi katika mkutano uliojumuisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali uliofanyika leo Jijini Dar Es Salaam.

Wadau mbalimbali wa Bima ya Afya kwa wananchi walio katika Sekta zisizo Rasmi wakisikiliza kwa makini mjadala uliokua ukiendelea katika mkutano uliojumuisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali uliofanyika Jijini Dar Es Salaam.

Waziri Ummy amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO) imefanya tathmini mbalimbali na kugundua watu wengi hawana uelewa wa masuala ya Bima ya Afya lakini wana uwezo wa kulipa. Kufuatia hali hiyo Serikali imeamua kuboresha mfuko wa afya wa jamii “CHF Iliyoboreshwa” kwa gharama nafuu kwa watu watano kwa mwaka ili kuwawezesha wananchi wengi kujiunga na mfuko huo.


“Hivi sasa asilimia 67 ya wananchi hawana Bima ya Afya, hivyo wanatumia fedha taslimu kupata huduma. Hii ni changamoto kwa wengi kwa kuwa matibabu yana gharama kubwa na ugonjwa huja bila taarifa”. Amesema Waziri Ummy.


Kikao hicho cha siku mbili kimejumuisha wajumbe kutoka nchi za Kenya, Congo, Ghana, Cameroon, Ethiopia, Ujerumani, Ufilipino, Chad, Zambia, Afrika Kusini, Uswisi pamoja na wenyeji Tanzania.
Loading...

No comments: