WATOTO 105 WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU WANUFAIKA NA HUDUMA ZA BIMA YA AFYA MKOANI MWANZA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, February 28, 2019

WATOTO 105 WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU WANUFAIKA NA HUDUMA ZA BIMA YA AFYA MKOANI MWANZA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.) akiwana watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi muda mfupi baada ya kuwakabidhi kadi za Bima ya matibabu kwa kwa hisani ya Benki ya STANBIC mkoa wa Mwanza.


Na mwandishi wetu Mwanza

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Ummy Ally Mwalimu amekabidhi Bima za Matibabu kwa watoto 105 wanaoishi katika mazingira magumu leo mkoani Mwanza.

Waziri Ummy alikabidhi vitambulisho hivyo vya Bima ya Afya kwa watoto hao kufuatia msaada ambao umetolewa na Benki ya STANBIC kwa watoto hao ili kuwawezesha kumudu na kutatua changamoto ya kimatibabu ambayo imekuwa ikiwakumba kwa muda mrefu.

Akitoa msaada huo, Waziri Ummy ameeleza kuwa Benki ya STANBIC imeonesha moyo ya kizalendo kwa kuwakumbuka na kuwalipia Bima za Afya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwemo yatima na kuongeza kuwa msaada wa bima ya mataibabu kwa watoto hao ni muhimu katika kuhakikisha kuwa wanapata malezi, makuzi na afya bora.

Aidha, Waziri Ummy amewashukuru watendaji wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuchukua hatua za haraka katika kuwasajili watoto hao waliopendekezwa na Wizara yenye dhamana ya maendeleo na ustawi wa watoto kwa umakini wao wa kukamilisha taratibu za utoaji wa vitambulisho vya Bima ya Afya kupitia ufadhili wa Benki hiyo.

Kuanzia Julai 2017 hadi Juni 2018 Tanzania ilikuwa na takribani watoto 864,496 wanaoishi katika mazingira magumu na kwa mkoa wa Mwanza peke yake una jumla ya  watoto 29,474 ambapo Benki hiyo imewezesha watoto 105 jambo ambalo ni zuri hivyo kutoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano wa Stanbic Bank.

Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa jumla ya watoto 6,132 walio katika Mazingira magumu walipatiwa huduma za msingi katika ‘makao ya watoto’ 157 yanayoendeshwa na Taasisi za dini, Mashirika ya watu binafsi na Serikali Nchini.

Aidha Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa katika idadi hiyo mkoa wa Mwanza peke yake una watoto 614 waishio katika makao hayo na kwa kupitia takwimu hizi ni dhahili kuwa Serikali na wadau wengine wa Maendeleo ya Mtoto tunao wajibu wa kuhakikisha watoto hawa wanaishi katika mazingira salama kwa kuzingatia ustawi na maendeleo yao.   

Waziri Ummy ametoa wito kwa Watanzania na wamiliki wa Makao ya kulelea watoto wenye shida kuzingatia Sheria na Kanuni za uendeshaji wa Makao ya Watoto  jambo ambalo litasaidia kuwa na Makao yanayotoa huduma bora za malezi na makuzi kwa watoto ambao wametoka kwenye shida mbalimbali.

Waziri Ummy amerejea kuupongeza uamuzi wa Benki ya STANBIC kwa kufadhili Bima za Matibabu za watoto 900 nchini, ambapo kwa Mkoa wa Mwanza watoto 105 wamenufaika. Uamuzi huu umekuja wakati muafaka ambapo Serikali ipo mbioni kupeleka muswada Bungeni wa Sheria ya Bima za Matibabu kwa Wananchi wote.

Bima ya afya ni suluhisho la utoaji wa huduma ya afya kwa kila mwananchi kabala ya kuugua na kufikishwa hospitalini hivyo ni muhimu kubadilika na kuchangia matibabu zaidi ya tunavyochangia huduma nyingine za kijamii.

MWISHO

Loading...

No comments: