Je kijana umejiandaaje na Uchaguzi mdogo 2019...? - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Saturday, March 2, 2019

Je kijana umejiandaaje na Uchaguzi mdogo 2019...?

Wakati tukiwa kwenye maandalizi ya uchaguzi mkuu Tanzania tuna mambo kadha wa kadha tungependa kushirikishana na vijana.

Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya mwaka 2012 asilimia 77% ya watanzania wana umri
ulio chini ya miaka 35 na asilimia 19% wana umri kati ya miaka 15–24.  Ifikapo 2020 tutakuwa na 40% ya wapiga kura wapya ambao watakuwa wanashiriki kwa mara ya kwanza.

Mwaka 2015 asasi za vijana hapa nchini kama vile YUNA, Restless Development, TYVA zilifanya tafiti kutambua mambo kadha wa kadha ya kuyapa kipaumbele kwa lengo la kuandaa ilani ya vijana. Katika ilani hiyo vijana waliweza kujadili mambo mbali mbali ambayo waliyapa kipaumbele kwenye kipindi cha miaka mitano ya awamu ya tano ambapo serikali mpya ilichaguliwa na wananchi.

Mambo kumi ambayo vijana  waliainisha  na kuyapa kipaumbele kulingana na uzito na umuhimu yalilenga ajira, elimu, huduma bora za afya, utawala bora na uwajibikaji, ushiriki na ushirikishwaji wa vijana, vijana na rasilimali, michezo sanaa na ubunifu, vijana wenye ulemavu, usawa wa kijinsia pamoja na vijana na diplomasia.  Malengo mengine katika ilani ni pamoja na kuainisha ushiriki wa vijana katika masuala mbalimbali ya kiraia na maoni yao juu ya mikakati mbalimbali ya maendeleo katika ngazi za serikali za mtaa, kitaifa na kimataifa katika kuwainua na kuwawezesha vijana na vilevile kuwasaidia vijana kupaza sauti zao juu ya masuala yanayowagusa.

Kwa kutambua umuhimu wa kundi hili na mchango wake katika kukuza ustawi wa taifa la Tanzania,
kuna umuhimu wa vijana kuwajibika na kujijengea uwezo katika kusimamia na kufuatilia maendeleo yao na pia kufanya utafiti baada ya kupata idhini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ambao utawawezesha kueleza hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa mikakati na mipango mbalimbali ya maendeleo inayowagusa na pia kutumia matokeo ya utafiti huu kuweza kupaza sauti, kushiriki katika kutoa maamuzi kwenye ngazi zote na kuongeza msukumo kwa wadau mbalimbali ikiwemo serikali, sekta binafsi na asasi za kiraia kuwekeza zaidi katika vijana.

Takwimu zilizofanywa na shirika la Restless Development zinaonyesha kuwa vijana 4 tu kati ya 10 wanasema kuna uwakilishi wa kutosha katika ngazi zote za mamuzi mfano katika mikutano ya mtaa/kijiji na halimashauri. Mwaka huu kama tunavyojua ni uchaguzi wa serikali za mtaa ambapo makala hii inajaribu kutoa elimu kwa vijana kushiriki katika kufanya maamuzi ya kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali pamoja na kupiga kura.

 Je kijana unayosoma makala hii umejiandaaje na huu uchaguzi? Je unafahamu nafasi yako na umuhimu wa kufanya maamuzi katika ngazi hii ya serikali za mtaa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu unaokuja? hayo ni baadhi ya maswali muhimu kama kijana unapaswa kujiuliza na kutambua kuwa sio mdogo kuwa kiongozi katika ngazi hii hata ngazi za kitaifa. Kufuatia ilani ya vijana iliyowekwa mwaka 2015 tumeona kuna vijana wengi wameingia kwenye nafasi mbali mbali za uongozi wa awamu ya tano, mfano mzuri ni Mheshimiwa mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah ambaye ni mkuu wa wilaya mdogo kwa sasa akifuatiwa na Mheshimiwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo ambaye pia ni damu changa katika uongozi wa awamu ya tano.

Vijana ni sauti muhimu kwenye kutoa maamizi na vijana wanaweza wakipewa nafasi, mwaka huu tunatarajia kuona vijana wengi zaidi wanapewa nafasi katika uongozi wa awamu ya sita. Ifikapo mwaka 2050 Tanzania itakuwa taifa la kwanza barani Afrika kuwa na vijana wengi zaidi wanakadiriwa. Matarajio yetu yote watanzania ni kuwa na dunia nzuri inayowategemea vijana. Maendeleo ya Malengo Endelevu (SDGs), haki za binadamu, pamoja na amani usalama vyaweza tu kupatikana  ikiwa tutawawezesha vijana  kama viongozi na kuwawezesha kutumia kikamilifu uwezo wao.

Usikose mwendelezo wa makala ijayo inayohusu mada ya vijana na uchaguzi wa serikali za mtaa mwaka 2019, jinsi vijana wanaweza kushiriki kwa kupiga kura na kufanya maamuzi ya kugombea..


Loading...

No comments: