KAGERE: TUTAWAFUNGA WAARABU JUMAMOSI
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba, Meddie Kagere, raia wa Rwanda, amewafuata wapinzani wao JS Saoura ya Algeria na matumaini kibao katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kusema kuwa anaamini watatinga hatua ya robo fainali.

Simba ipo nafasi ya pili ya msimamo katika Kundi D ya Ligi ya Mabingwa ikiwa na pointi sita, inatarajiwa kushuka dimbani siku ya Jumamosi wiki hii kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Saoura ambapo katika mchezo wa awali walifanikiwa kuwafunga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar hivyo mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani zaidi.

Kikosi cha Simba kimeondoka jana mchana kuelekea nchini Algeria kikiwa na msafara wa wachezaji 20. Akizungumza na Championi Jumatano, Kagere ambaye ndiye kinara wa mabao ndani ya Simba kwa sasa, amesema kuwa, amejiandaa vyema kuelekea katika mchezo huo na kudai kuwa iwapo Wanasimba wataungana kwa pamoja, kuna uwezekano mkubwa wa kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

“Kwa sasa tumegeukia michuano ya kimataifa tunajiandaa na mchezo wetu dhidi ya Saoura, tunawaomba wapenzi wote wa Simba na wasiokuwa Simba tuungane kwa pamoja kuiombea timu yetu kwani tukifanya hivyo tunaweza kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali, nusu fainali na hata fainali.

“Tunaomba tuungane kwa kuomba katika mchezo wetu dhidi ya Saoura ili tuweze kufanya vizuri kisha tuje kumalizia mchezo wetu hapa nchini na AS Vita ili tushinde na kutinga hatua ya robo fainali, kwa pamoja tunaweza kulifanikisha hilo. 

“Nimejiandaa vizuri kupitia mazoezi ya mwalimu pia namuomba Mungu tuweze kufanikiwa kufanya vizuri katika mchezo huo,” alisema Kagere.

Post a Comment

0 Comments