KIKONGWE AUAWA KWA TUHUMA ZA KUROGA MVUA ISINYESHE WILAYANI KILINDI, TANGA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, March 7, 2019

KIKONGWE AUAWA KWA TUHUMA ZA KUROGA MVUA ISINYESHE WILAYANI KILINDI, TANGA


Tafrani imeibuka katika kijiji cha Ngeze wilayani hapa baada ya watu wanaodaiwa kuwa na hasira kumuua Mzee Dimon Senyagwa (85) kwa kumshambulia kwa mawe na silaha nyingine za jadi wakimtuhumu kuzuia mvua isinyeshe.

Wananchi hao walimtuhumu Mzee Dimon kuwa anatumia njia za kishirikina kuzuia mvua isinyeshe kijijini hapo ili mazao mbalimbali yaliyopandwa yanyauke.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe ni kwamba mzee huyo aliuawa Jumapili saa 11:00 jioni kijijini hapo kata ya Kwekivu, tarafa ya Kwekivu wilayani hapa.

Mashuhuda wa tukio hilo walilieleza Mwananchi kuwa tukio hilo lilitokea baada ya baadhi ya wanakijiji kutangaza kwamba mvua hainyeshi kijijini hapo kwa sababu ya Mzee Senyagwa.

“Baada ya habari hizo kuenea kijijini likaibuka kundi la vijana wakaamua kumfuata nyumbani kwake na kuanza kumshambulia wakidai anaroga mvua,” alieleza Hussein Lucas.

Kufuatia mauaji hayo, Mwananchi ilifahamishwa kuwa baadhi ya vijana wamekimbilia msituni wakitoroka kukamatwa kwa kuhusishwa na tukio hilo.

Akizungumzia tukio hilo, kamanda Bukombe alisema watu sita wanashikiliwa wakituhumiwa kuratibu na kutekeleza mashambulizi ya mauaji hayo.

“Nitoe tamko langu kwa msisitizo mkubwa, tabia hii ya kuamini mambo ya kishirikina inatakiwa kupigwa vita, polisi tutapambana na ambao wanaamini ushirikina huu maeneo yote ya mkoa,” alisema Bukombe.

Bukombe aliwataka wananchi kutii sheria bila shuruti na kuachana na imani za aina hiyo ambazo zimepitwa na wakati, kwani mtu kuwa na umri mrefu siyo kwamba ni mchawi.

CHANZO: Mwananchi 
Loading...

No comments: