Mabadiliko Yanayotokea Kwenye Mwili na Afya Yako Baada ya Kuanza Mazoezi! - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, March 5, 2019

Mabadiliko Yanayotokea Kwenye Mwili na Afya Yako Baada ya Kuanza Mazoezi!

Kufanya mazoezi mara kwa mara hufanya mabadiliko makubwa ndani na nje ya mwili wako. Baada ya kufanya mazoezi kwa mara ya kwanza unaweza kuhisi mwili umechangamka kwa sababu mapigo ya moyo huongezeka kitu kinachomaanisha ongezeko la mzunguko mkubwa wa damu na oksijeni kwenye ubongo. Lakini jiandae na maumivu ya viungo baada ya siku moja, maumivu yanaweza kuwepo hadi masaa 72 hata hivyo huwezi kupata tena hali hiyo ukiendelea na mazoezi.


Baada ya wiki kadhaa za mazoezi mwili utaanza kutengeneza mitokondria. Mitokondria ni oganeli ndogondogo katika sitoplazimu ya seli ambazo hutengeneza nishati inayotumika katika seli. Mitokondria hubadili wanga, mafuta na protini kuwa nishati inayotumiwa na mwili kufanya shughuli mbalimbali.

Kulingana na tafiti baada ya wiki 6 hadi 8 za mazoezi, mitokondria huongezeka hadi kufikia 50%. Kuwa na mitokondria nyingi kwenye seli zako, utajihisi sawa (fit) na stamina huongezeka, hivyo kukimbia maili tatu hakutaonekana kugumu kama ilivyokuwa wiki ya kwanza.


Ikiwa utafanya mazoezi mfululizo kwa miezi 6, utaona matunda ya mazoezi unayofanya. Ikiwa unafanya mazoezi ya kubeba vitu vizito misuli yako itaanza kutengeneza umbo la kimazoezi. Angalau 50% ya watu huacha programu za mazoezi na ambao huendelea huwa wafuasi wazuri wa mazoezi.


Ikiwa imejikita kwenye mazoezi ya moyo, hadi kufikia miezi 9 ya mazoezi ya ukawaida utaweza kuona ongezeko la 25% la hewa safi kwenye mzunguko wa damu. Kuwa na mzunguko mzuri wa oksijeni hufanya misuli kupata nguvu zaidi hii inaweza kumsaidia mtu kukimbia kwa kasi kubwa na kwa muda mrefu.Baada ya mwaka mmoja wa mazoezi kwa ukawaida mifupa yako huwa minene na kupunguza hatari ya osteoporosisi (aina ya kusinyaa kwa mifupa ya sehemu moja au mifupa yote mwilini ambapo tishu ya mfupa hupotea lakini bila ya kuathiri muundo wa mfupa mzima). Watafiti pia wamedai kwa wale tayari wana tatizo hilo wakiweza kufanya mazoezi yanayojumuisha kujenga stamina mfano kubeba vitu vizito na aerobiki mfano kukimbia wanaweza ondoa tatizo hilo baada ya miezi 12 ya mazoezi kwa ukawaida.

Kwa kuendelea kufanya mazoezi kwa kipindi kirefu unaweza kuwa na afya bora na kuepuka gharama za matibabu hivyo kutunza fedha zaidi kwa ajili ya shughuli zingine. Pia utapunguza hatari ya magonjwa kama arthritisi (kuvimba vifundo vya mifupa), kisukari, saratani na kupanda kwa shinikizo la damu, hii itakusaidia kuishi umri mrefu zaidi na kutimiza mengi.

Pia, utaridhika na maisha na kuwa na furaha kwa maana mazoezi hupunguza wasiwasi (anxiety) na huzuni kubwa (depression) kwa kupunguza viwango vya homoni za mkazo (stress) kama cortisol na adrenalini.


Ili kufurahia faida hizo za mazoezi ni vyema kula mlo kamili. Kwa mtu mwenye 18-64 wataalamu wa mazoezi wanapendekeza kufanya mazoezi mepesi kama kuendesha baiskeli angalau masaa mawili na nusu kwa wiki. Au mchanganyiko wa mazoezi mepesi na magumu kama kuogelea na kukimbia kwa angalau saa moja na dakika 15 kila wiki.


Juu ya hayo mazoezi, hakikisha unatumia siku mbili kila wiki kuimarisha misuli yako kwa kufanya mazoezi kama kubeba uzito mkubwa. Hii itakuimarisha na kukuongezea kasi. Utashangaa baada ya muda unaweza kukimbia hata mbio ndefu (marathon).
Loading...

No comments: