Mkutano Mkuu wa ‘CUF Lipumba’ kesho, wajumbe waanza kuwasili - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, March 11, 2019

Mkutano Mkuu wa ‘CUF Lipumba’ kesho, wajumbe waanza kuwasili
Mmoja wa mkutano mkuu waChama cha Wananchi (CUF)akiandikisha jina kwa ajili ta kusubiri  utaratibu wa mkutano mkuu wa chama hicho 
By Bakari Kiango, Mwananchi bkiango@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF), upande unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama hicho, anayetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba umesema maandalizi ya mkutano mkuu wa siku tatu uliopangwa kufanyika kesho Jumanne Machi 12, 2019 yamekamilika.
Kauli hiyo imetolewa leo, Jumatatu Machi 11, 2019 na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Abdul Kambaya wakati akizungumza na Mwananchi katika ofisi ya makao makuu ya CUF iliyopo Buguruni.


Amesema kila kitu kinakwenda vizuri na wajumbe wa mkutano huo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wameanza kuwasili kwa ajili ya kushiriki mkutano huo na kuwataka wasitishike na vitisho vinavyotolewa na baadhi ya wanaosema mkutano hautafanyika.
"Mkutano utaanza kesho na utafanyika katika mojawapo ya hoteli iliyopo karibu na ofisi ya makao makuu ya chama hiki.”
“Kwa asilimia kubwa wajumbe wameshafika kama ambavyo umeona wakati ukiingia humu ndani," amesema Kambaya.


Mwananchi imeshuhudia baadhi ya mabasi yakipishana katika ofisi hiyo kwa ajili ya kushusha wajumbe mbalimbali hasa wanaotoka Ungujar kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo wa kesho.
Baadhi ya wanachama walisikika wakisema  "hiyo ni timu kutoka Unguja imeshawasili eeh Mungu tujaalie tumalize salama mkutano huo na itakuwa ndio mwisho wa Maalim Seif Sharif Hamad na watu wake.”


Mkutano mkuu huo licha ya kujadili masuala mengine lakini utafanyika uchaguzi wa kujaza nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo ya mwenyekiti na katibu mkuu.
Kwa mujibu wa Kambaya, mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe zaidi ya 700 na wadau mbalimbali wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali ingawa hakuwataja hadharani.

Alipoulizwa endapo wamewaalika baadhi ya vyama vya siasa kushiriki kama ilivyo desturi Kambaya amesema " Hatujawaalika hao watu, kama tutaona umuhimu wa kualika tutafanya hivyo lakini kwa sasa hakuna aliyealikwa.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, kutoka Kanda ya Kusini, Hawa Shaaban amesema mkutano mkuu huo utafanikiwa kwa asilimia 100 kutokana na maandalizi yaliyofanyika na wanatarajia kupata viongozi wapya.


CHANZO; MWANANCHI
Loading...

No comments: