MOSHI: RAIA WA LIBERIA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA KWA KUSAFIRISHA MADAWA YA KULEVYA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, March 8, 2019

MOSHI: RAIA WA LIBERIA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA KWA KUSAFIRISHA MADAWA YA KULEVYA


Raia wa Liberia, Bi Grace Teta mwenye umri wa miaka 40, maisha yake yamehamia gerezani atakakokutumikia kifungo kwa uhai wake wote. 

Grace, aliyehukumiwa kifungo hicho jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi chini ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Patricia Fikirini, alikamatwa Desemba Mosi, 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akisafirisha gramu 10,064 za dawa za kulevya aina ya heroini. 

Upande wa mashtaka uliojumuisha mawakili wanne wa Serikali uliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa huyo alikuwa akisafirisha dawa hizo kwenda Free Town, Liberia kupitia Nairobi, Kenya.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Fikirini alisema Mahakama imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi tisa na vielelezo 13 vilivyowasilishwa na upande wa mashtaka ambao haukuacha shaka. 

Ilielezwa kuwa wakati akiwa katika ukaguzi uwanjani hapo, maofisa wa usalama walimtilia shaka na kumfanyia ukaguzi uliobaini ndani ya kila begi kati ya mawili aliyokuwa nayo kulikuwa na kibegi kidogo cheusi vilivyokuwa na dawa hizo. 

Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka, mshtakiwa alipohojiwa katika kituo cha polisi KIA na ofisi ya upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro alidaiwa kukiri kusafirisha dawa hizo. 

Loading...

No comments: