NI RASMI SASA MADRID & DORTMUND NJE UEFA, WAKUBALI VICHAPO NYUMBANI KWAO - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Wednesday, March 6, 2019

NI RASMI SASA MADRID & DORTMUND NJE UEFA, WAKUBALI VICHAPO NYUMBANI KWAO


"Mende kaangusha kabati" ndio msemo pekee unaoweza kuutumia kuelezea kile kilichotokea jana hasa katika uwanja wa Santiago Bernabeu ambapo wenyeji na mabingwa watetezi mara tatu mfululizo Real Madrid waliwakaribisha AJAX kutoka uholanzi huku wakiwa wanaongoza kwa magoli 2-1 waliyoyapata katika mechi ya kwanza kule Uholanzi. 

Hakuna ambaye aliwapa nafasi kubwa Ajax kufanya kile walichokifanya hasa kwasababu hawana rekodi nzuri dhidi ya miamba hiyo ya Hispania na walikuwa wanaenda kucheza kwenye uwanja wa Madrid. 

Wachezaji wa timu ya AJAX wakishangilia ushindi wao hapo jana baada ya mechi kuisha.
Lakini kilichotokea kimekuwa ni tofauti sana kwani Ajax wameuthibitishia Ulimwengu kuwa "MPIRA UNADUNDA" baada ya kuwachapa Madrid 4-1 hapo jana usiku katika uwanja wao. Magoli ya Ajax yalifungwa na Hakim Ziyech dakika ya 7, David Neres dakika ya 18, Dusan Tadic dakika ya 62, na Lasse Schonne dakika ya 72. Goli la kufutia machozi la Real Madrid lilifungwa na kinda Marco Asensio dakika ya 70. 

Upande wa pili kule Ujerumani kulikuwa na mechi kali pia kati ya wenyeji Borussia Dortmund dhidi ya Tottenham Hotspurs ambao walishinda 3-0 katika mechi ya kwanza kule kwao Uingereza. Katika mechi hii tulitegemea kuiona ile Dortmund ambayo huwa inageuza matokeo ikifanya mambo yake lakini sicho kilichotokea. 

Nahodha na winga wa Borussia Dortmund Marco Reus akizuiwa kupiga shuti na beki wa Tottenham Hotspurs Vertoghen katika mechi yao iliyoisha kwa Spurs kushinda 1-0. 
Dortmund walicheza mpira mwingi sana lakini hawakuwa waangalifu katika kutumia nafasi walizokuwa wanazitengeneza na pia ubora wa safu ya ulinzi ya Tottenham uliwazuia kufanya madhara yoyote. Walipiga mashuti 19 kwa ujumla huku mashuti 7 tu yakilenga goli wakati Spurs wao kwa ujumla walipiga mashuti 5 tu na shuti 1 tu ndio lililenga goli na ndio likawa goli lililoamua matokeo ya mechi hiyo. 

Mechi iliisha kwa Spurs kuibuka washindi kwa 1-0 goli la Harry Kane dakika ya 48. 

Kwa matokeo hayo ya mechi hizo mbili, ni rasmi sasa kuwa mabingwa watetezi Real Madrid pamoja na Borussia Dortmund wametupwa nje ya mashindano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya. Pia ni rasmi sasa kuwa AJAX AMSTERDAM pamoja na TOTTENHAM HOTSPURS zinakuwa timu za kwanza kabisa kutinga hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa msimu huu 2018/2019. 

Michuano hiyo inaendelea leo kwa kuzikutanisha timu zifuatazo:
  • FC PORTO VS AS ROMA (1-2)
  • PSG VS MAN UNITED (2-0)

Nani atajiunga na Ajax na Spurs kwenye robo fainali hii leo? 
Loading...

No comments: