Serikali yakanusha kuuzwa kwa ndege yake ya Aibus A 220-300 - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Sunday, March 31, 2019

Serikali yakanusha kuuzwa kwa ndege yake ya Aibus A 220-300


Serikali yakanusha kuuzwa kwa ndege yake ya Aibus A 220-300
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) imekanusha uvumi uliosambazwa kwenye mitandao ya jamii kuwa ndege yake mpya ya Airbus A 220-300 iko kwenye mchakato wa kuuzwa nchini Kenya baada ya nchi kukosa vibali vya kuiruhusu kwenda nje ya nchi.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa ATCL, Josephat Kagirwa alisema kuwa madai hayo hayana ukweli wowote na kuwataka Watanzania kuupuuza kwani yamefanywa kuichafua nchi. Kagirwa alikiri kuwa ndege hiyo ya A220-300 juzi ilikwenda nchini Kenya baada ya kukodiwa kibiashara na ilirudi siku hiyo hiyo na jana iliendelea na ruti zake kama kawaida.

Jana (juzi) A220-300 ilikodishwa kibiashara kwenda Kenya, lakini ilirudi siku hiyo hiyo na leo (jana) imeendelea na operesheni zake kama kawaida, hivyo madai ya kwamba inauzwa sio ya kweli, wananchi wayapuuze,” alisema Mkuu huyo wa Mawasiliano wa ATCL.

Ndege ya A 220-300 ni ndege mpya na za kisasa ambazo kwa Bara la Afrika, Tanzania ndio nchi pekee kuwa nazo zikiwa na uwezo wa kubeba abiria 132. Daraja la kwanza ni abiria 12 na la kawaida ni abiria 120. A220-300 ilinunuliwa nchini Canada na hiyo ni moja ya juhudi za serikali za kuimarisha usafiri wa anga na kwa mara ya kwanza iliruka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA), kutua nchini Zimbabwe na Zambia mapema mwezi uliopita. Airbus ikiwa nchini Zimbabwe na Zambia ilifanyiwa uzinduzi Uwanja wa Robert Gabriel Mugabe mjini Harare, na Uwanja wa Kenneth Kaunda jijini Lusaka.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema ATCL imedhamiria kujiimarisha katika sekta hiyo kwa kuongeza idadi ya ndege ikiwamo kufika nchi nyingine za Afrika na Bara la Asia.

Loading...

No comments: