UGONJWA WA KISUKARI WAONGOZA KWA KUPOTEZA VIUNGO - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, March 22, 2019

UGONJWA WA KISUKARI WAONGOZA KWA KUPOTEZA VIUNGO

Mkuu wa Kitengo cha Vifaa Tiba Saidizi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dk. Leah Mamseri amelieleza gazeti la Mtanzania kuwa ugonjwa wa kisukari kwa sasa unaongoza kutesa mamima na wengi wao wakijikuta wakipoteza viungo na kuhitaji vifaa tiba saidizi.


 Dk. Leah Mamseri amesema kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika katika kitengo hicho kwa sasa kuhitaji viungo bandia ni wagonjwa wa kisukari na kuwa ugonjwa huo unaongoza baada ya kudhibitiwa kwa ajali za barabarani ambazo awali ndizo zilikuwa zikiongoza.

 “Idadi kubwa ya wagonjwa wenye kuhitaji vifaa saidizi vikiwamo viungo bandia ni wale wenye kisukari baada ya kudhibitiwa ajali za barabarani,” alisema Dk. Leah.

Ameeleza sababu nyingine inayosababisha watu kuhitaji vifaa saidizi ni kupooza kutokana na baadhi ya mishipa ya fahamu kupoteza uwezo wake wa kufanya kazi.

 “Kuna watoto wanaozaliwa wakiwa na upungufu wa viungo, ajali za moto na za viwandani, kuumwa na nyoka, nazo huchangia kuhitaji vifaa tiba,” alisema Dk. Leah.

Aliwashauri waliopoteza viungo vyao kutokata tamaa ya maisha bali wafike hospitalini kupatiwa viungo saidizi waendelee na maisha yao kama ilivyokuwa awali.

 “Niwashauri Watanzania kubadili mfumo wa maisha yao kwa kula vyakula vya asili na kufanya mazoezi kuepuka wagonjwa ya kisukari na kupooza,” alisema.

Wakati huohuo, Dk. Leah amewataka watu wenye mahitaji ya viungo saidizi kujiorodhesha hospitalini hapo waweze kupatiwa viungo hivyo bure na Taasisi ya BMVSS kutoka India.

Alisema taasisi hiyo itaweka kambi nchini na kuwapatia viungo na vifaa saidizi watu 600. “Niwaombe wenye mahitaji wajitokeze kujiorodhesha wapatiwe huduma hii bure kwa sababu bima hazina mafao yanayoweza kulipia viungo hivi,” alisema Dk. Leah.

 DALILI ZA KISUKARI 


Watu wenye kisukari wapo katika hatari zaidi ya kupatwa na magonjwa ya moyo, kiharusi, matatizo na kuharibika kibofu cha mkojo, shinikizo la juu la damu, upofu, kufa neva za fahamu, uharibifu katika fizi na ugonjwa wa fangasi.

Mtu anapokuwa na kisukari, mzunguko wa damu miguuni hupungua na ndiyo sababu kubwa ya kufa neva za fahamu na hivyo mtu kukosa hisia katika eneo hilo la mwili. Matokeo ya hali hiyo ya kutohisi punde mtu anapodhurika na kusababisha kidonda ambacho mara nyingi mhusika anakuwa hafahamu hadi anapofahamishwa na mtu wa karibu au atakapokagua miguu yake.

Hii ni moja ya sababu kubwa ya watu kushauriwa kukagua miguu yao kila siku kabla ya kulala kuona kama kuna mchubuko wa aina yoyote au ukucha unaoweza kuchimba ngozi. Kutokuzingatia masharti ya kujikagua huweza kusababisha kidonda kukua, kutotibika na hatimaye mgonjwa kuishia kupoteza kidole, unyayo au hata mguu.

 JINSI YA KUZUIA 


Vile vile, kutokuzingatia masharti ya kujua kiwango cha sukari mwilini huweza kusababisha mtu akapoteza fahamu kutokana na mwili kuzidiwa sukari asidi (diabetic ketoacidosis), na hii huweza kusababisha kifo.

 Mgonjwa anaweza kuzuia madhara yatokanayo na kisukari kwa kuzingatia maelekezo, masharti na ushauri wa wahudumu wa afya, hasa kuhusu chakula na mazoezi na maelekezo ya matumizi sahihi ya dawa au insulin.

Mgonjwa hatakiwi kuvuta sigara, awe anapima kiwango chake cha shinikizo la damu mara kwa mara na kuhakikisha kiwango chake cha lehemu kipo katika uwiano unaotakiwa.

 Takwimu zinaonyesha uzingatiaji wa hayo yaliyotajwa umesaidia watu wengi kupunguza madhara ya kisukari kwa asilimia 75.

Lishe mahsusi kwa mtu mwenye kisukari ni mlo wenye kiwango kidogo cha mafuta, kiwango kidogo cha chumvi na kiwango kidogo cha sukari. Mlo uwe na mchanganyiko wa nyuzinyuzi kama vile dona (unga wa mahindi yasiyokobolewa), nafaka, tambi, ndizi za kupika, mtama, uwele.

Vile vile matunda machachu na mboga za majani zinazolimwa na zile za porini zinazoliwa kama mchunga, tembele, majani ya maboga, majani ya kunde na mbilimbi.

Ni vema kujitahidi kula kiasi kidogo cha chakula walau mara tano kwa siku kuliko mlo mkubwa mara mbili au tatu kwa siku.

 Taarifa hii imeadikwa na Glory Lyamuya (Dsj) Na Tunu kupitia Mtanzania online

Loading...

No comments: