VURUGU TAIFA ZASABABISHA KIFO CHA MTOTO WA MIAKA SABA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, March 25, 2019

VURUGU TAIFA ZASABABISHA KIFO CHA MTOTO WA MIAKA SABA

Dar es Salaam. Mtoto Ibrahim Hassan (7) amefariki dunia baada ya kukanyagwa na mashabiki jana Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Temeke.
Vurugu hizo zilitokea jana Uwanja wa Taifa wakati wa mchezo kati ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Machi 25, 2019 muuguzi wa zamu Hospitali ya Temeke, Rolester Kinunda amesema walipokea watu 18 waliopata majeraha kwenye vurugu zilizotokea Uwanja wa Taifa.
Amesema miongoni mwa majeruhi hao ni watoto watatu akiwamo Ibrahim Hassan aliyefariki dunia kwa kukanyagwa na wananchi.
Amewataja watoto wengine ni Ibrahim Said Omary (13) na Joseph Paulo (14).
"Wote ukiachilia aliyefariki, walipata michubuko na wengine walikuwa wakilalamika kupata maumivu ya kifua, walipimwa na kuonekana hawajaumia ndani, hivyo walipatiwa dawa za maumivu na kuruhusiwa," amesema Kinunda.
Kwa upande wa baba wa mtoto aliyefariki Hassan Ibrahim amesema (huku akilia sana) kuwa mapenzi kwa mwanaye yameondoa furaha yake.
"Nilikuwa nampenda sana mwanangu, sikuwa na fedha ya kulipia kuingia uwanjani, lakini kwa sababu alitaka aone hata kwa nje na kwa sababu nampenda sana nilikubali ombi lake.”
"Baada ya kufika uwanjani geti likafunguliwa nikaona kama watu wanaingia bure, tukaingia, lakini vurugu zikawa nyingi nikaona nimdake mwanangu tutoke, dada mmoja akaanguka, nikajikwaa na kumuangukia na watu wengi wakaja juu yangu...kitu pekee nilichosikia kutoka kwa mwanangu (kilio) baba nakufa," amesema Hassan.
Amesema baada ya hapo hakuwa na fahamu hadi alipojikuta yupo ndani ya gari ya polisi akiwa hana fahamu na kupelekwa Hospitali ya Temeke.
 
"Nilimuona dada nisiyemjua akiwa amempakata mwanangu huku amemfunika kitenge, sikuwa na shaka nilijua atapona baada ya kupatiwa matibabu, mimi pamoja na majeruhi wengine tulipokelewa kwa ajili ya matibabu (kilio) baada ya muda naambiwa mwanangu amefariki...uwiii ( anavua jaketi na kulia kwa sauti).

Chanzo: Mwanachi
Loading...

No comments: