ALIYEMUUA MPENZI WAKE HOSTELI ZA MABIBO AHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA. - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, April 1, 2019

ALIYEMUUA MPENZI WAKE HOSTELI ZA MABIBO AHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA.


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemhukumu kunyongwa hadi kufa Masamba Musiba (39) aliyepatikana na hatia ya mauaji katika kesi ya kumuua mpenzi wake, Betha Mwarabu katika hosteli za Mabibo jijini Dar es Salaam.

Mshitakiwa pamoja na Betha walikuwa ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wakiishi katika hosteli hizo. Mauaji hayo yalitokea Juni 6, 2009 katika hosteli hizo zilizoko Wilaya ya Kinondoni. Siku ya tukio, saa tatu usiku katika hosteli hizo, mshitakiwa alikwenda katika chumba namba 250 cha mpenzi wake ambaye sasa ni marehemu Betha.

Mshitakiwa aliongea na mpenzi wake huyo na ghafla alitoa kisu na kuanza kumchoma kifuani, alianguka chini na baadaye alisaidiwa na wanafunzi wenzake baada ya kusikia akipiga kelele, mshitakiwa alikimbia. Akitoa hukumu hiyo juzi, Jaji wa Mahakama Kuu, Elvin Mugeta alisema mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka bila kuacha shaka yoyote, ambako alisema pia kuwa hakuona sababu ya mshitakiwa kusingiziwa shitaka hilo.

“Mashahidi waliomuona kwenye tukio walimtambua vizuri na hawakuwa na sababu yoyote ya kumsingizia, kwa hiyo Mahakama inamuona mshitakiwa ana hatia ya mauaji ya kukusudia na hivyo inamhukumu kunyongwa hadi kufa,” alisema Jaji Mugeta katika uamuzi wake.

Mshitakiwa baada ya kukamatwa, kesi yake ilifunguliwa katika Mahakama ya Kinondoni kwa mara ya kwanza, lakini baadaye aliachiwa na kukamatwa tena Mei 25, 2015 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alisomewa tena mashitaka ya mauaji.

Uchunguzi wa awali wa kesi hiyo ulikamilika Mei 25, 2016 katika Mahakama ya Kisutu na kesi yake kuhamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza kusikilizwa. Agosti 15, 2016 ilianza kusikilizwa ambako upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi watano waliotoa ushahidi mahakamani na pia uliwasilisha vielelezo vinne vya nyaraka pamoja na kisu. Hata hivyo, mshitakiwa alijitetea peke yake hakuwa na shahidi.

Akichambua ushahidi huo, Jaji Mugeta alisema anakubaliana na ushahidi wa upande wa mashitaka kwa kuwa mashahidi wa upande wa Jamhuri walimtambua vizuri mshitakiwa na hawakuwa na sababu yoyote ya kumsingizia.

Ushahidi wa Flora Chengula ambaye alikuwa akiishi hosteli moja na mshitakiwa pamoja na Betha, alikiri kumfahamu mshitakiwa ambapo alisema alikuwa akiwaona pamoja na Betha mara kwa mara.

Siku ya tukio alisema alipita na kuwakuta mshitakiwa pamoja na mpenzi wake wakiwa katika chumba cha dada huyo katika hosteli hizo, baadaye alisikia kelele ambazo zilipigwa na Betha, alipokwenda kuangalia alikuta akiwa amelala chini na amechomwa na kitu.

Alichukuliwa akiwa katika hali mbaya kupelekwa hospitali, lakini alifariki akiwa njiani na uchunguzi kufanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Ushahidi uliotolewa na mlinzi katika zahanati ya hosteli hizo, alisema mshitakiwa alikamatwa akijaribu kutoroka akiwa na begi, watu walitaka kumpiga aliomba karatasi na kalamu alipopewa aliandika ujumbe kuwa ‘Betha mpenzi wangu naomba nisamehe.’

Alichukuliwa na askari na kupelekwa Kituo cha Polisi Urafiki. Katika utetezi wa mshitakiwa, alikana kukamatwa siku hiyo saa tatu usiku, alisema muda huo alikuwa ameshakamatwa kwani siku hiyo alikamatwa saa tisa mchana baada ya mwanafunzi mwenzake alimsingizia kuwa alimuibia kompyuta ya mkononi.

Alikana pia begi alilokamatwa nalo ambapo alisema vitu vilivyokutwa kwenye begi hilo ambavyo ni vyeti vyake vya shule, picha yake na ya mpenzi wake huyo pamoja na nguo kuwa alikua ameviweka chumbani kwake hosteli vimechukuliwa huko na askari. Jaji Mugeta alisema Masamba ana uhuru wa kukata rufaa kama hakuridhika na uamuzi huo.
Loading...

No comments: