Atoka Gerezani na Kushangaa Smartphone Baada ya Kukaa Miaka 30


Atoka gerezani na kushangaa smartphone baada ya kukaa miaka 30
Mkazi wa Usangi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, Kassim Mbaga amemaliza kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Hata hivyo, Mbaga ambaye kimahesabu amekaa jela miaka 24 jambo ambalo limemshangaza katika maisha ya mtaani ni kukutana na simu janja (smart phone).

Mbaga alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la wizi wa kutumia nguvu mwaka 1995 na aliingia gerezani akiwa kijana wa miaka 23 na kutoka jela akiwa na umri wa miaka 47.

Mbaga aliwasihi Watanzania kuheshimu sheria za nchi na kuachana na matendo maovu kwani kama wataenda gerezani, wajue watarudi nyuma kimaendeleo.

“Mimi nilienda gerezani nikiwa kijana mdogo sana, nikiwa na miaka 23. Miaka niliyokaa huko kama ningekuwa uraiani ningekuwa nimeshafanya shughuli nyingi za kimaendeleo,” alieleza Mbaga.

Mbaga alisema baada ya kuachiwa huru Januari 21, alishangaa vitu alivyokutana navyo ikiwemo simu janja (smartphone) na mfumo wa analojia kubadilika na kwenda digitali.

“Niliporudi kijijini nilishangaa kila mtu ana smartphone. Yaani wenye simu za batani ni wachache. Nimekuta nyumba za kifahari huku kijijini nikaona kumbe na mimi nilipotezea muda.

“Nashangaa sasa hakuna ugonjwa wa malaria ila presha na kisukari ndio ugonjwa unaowasumbua watu huku mtaani, hata wengi waliokufa nasikia wamekufa kwa magonjwa hayo,” alisema.

Kilichomponza Mbaga alisema chanzo cha yeye kwenda jela ni ugomvi kati yake na mtoto wa mama yake mdogo ambao ulizuka mwaka 1994 wakiwa katika mazungumzo ya kazi.

Alisema kosa hilo lilipelekwa mahakamani na zilifunguliwa kesi tano kwa wakati tofauti na baadaye kukamatwa tena kwa kosa jingine la wizi wa kutumia nguvu.

“Kesi nne zilifutwa na kesi ya tano ya wizi wa kutumia nguvu ndio niliyohukumiwa nayo kifungo hicho. Nilishtakiwa kwa kuiba, wizi wa uaminifu, kuvunja na kuiba na wizi wa kutumia nguvu,” alisema.

Mbaga alisema “kwakuwa sikuridhika na hukumu nilikata rufaa mara tatu ila nilishindwa kesi hiyo na nikaendelea kutumikia kifungo changu ambacho nilimaliza mwezi Januari mwaka huu,” alisema. 

Post a Comment

0 Comments