BUNGE LAAZIMIA KUTOFANYA KAZI NA CAG, HALIMA MDEE AFUNGIWA, WABUNGE WA UPINZANI WATOKA NJE - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, April 2, 2019

BUNGE LAAZIMIA KUTOFANYA KAZI NA CAG, HALIMA MDEE AFUNGIWA, WABUNGE WA UPINZANI WATOKA NJE

Dodoma: Leo Jumanne Aprili 2, 2019 Bunge limepitisha azimio la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.Uamuzi huo umepitishwa baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki,  Maadili na Madaraka ya Bunge,  Emmanuel Mwakasaka kuwasilisha na kusoma bungeni taarifa ya kamati hiyo iliyomhoji CAG,  kumtia hatiani baada ya kubaini kauli aliyoitoa kuwa Bunge ni dhaifu,  amelidhalilisha Bunge.

Kabla ya kupitisha azimio hilo Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alitoa nafasi kwa wabunge kujadili jambo hilo huku wabunge wakipishana maoni yao,   kukubaliana na uamuzi huo na wengine kupinga akiwemo Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe.


Katika hatua nyingine Bunge limeridhia mapendekezo ya  Kamati ya Bunge ya  Haki,  Maadili na Madaraka ya Bunge kumsimamisha mbunge wa Kawe (Chadema),  Halima Mdee kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kuanzia tarehe ya azimio hilo kutokana na kuunga mkono kauli ya CAG.

Baada ya wabunge kuchangia mapendekezo ya Kamati ya Bunge kuhusu mbunge huyo wa Kawe, alilihoji Bunge na kupitisha azimio la Mdee kutoshiriki mikutano miwili ya Bunge.

"Bunge limeazimia kuwa Mdee hatashiriki mkutano huu (wa Bajeti)  wa 15 wa Bunge na mkutano wa 16 utakaofanyika Septemba na Oktoba, 2019," amesema Dk Tulia.


Wakati wa mjadala Dk Tulia Ackson aliagiza Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kutamka bungeni kuwa Bunge ni dhaifu.

Dk Tulia amechukua uamuzi huo baada ya Lema wakati akichangia hoja ya kamati hiyo kudai Halima Mdee hajatendewa haki kutokana na kamati hiyo kupendekeza Bunge kumsimamisha kuhudhuria vikao viwili vya Bunge kutokana na kuunga mkono kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuwa Bunge ni dhaifu.

"Alichokisema Mdee naungana naye na nikweli kuwa Bunge ni dhaifu," amesema Lema. Baada ya kauli hiyo Dk Tulia aliagiza Lema kuhojiwa na kamati hiyo kuthibitisha kuwa kweli Bunge ni dhaifu, kauli ambayo iliwanyanyua wabunge hao.

Uamuzi huo umesababisha wabunge wa upinzani kunyanyuka walipokuwa wameketi na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge. Waliotoka nje ni wabunge wa Chadema na baadhi ya wabunge wa CUF.


KAMATI: BUNGE HALIKO TAYARI KUFANYA KAZI NA CAGLoading...

No comments: