DAKTARI FEKI ASAKWA KWA KUSABABISHA KIFO WAKATI AKITIBU IGUNGA-TABORA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, April 30, 2019

DAKTARI FEKI ASAKWA KWA KUSABABISHA KIFO WAKATI AKITIBU IGUNGA-TABORA


KAMATI ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Igunga mkoani Tabora inamtafuta daktari feki Emmanuel Peter (50), mkazi wa kitongoji cha Mwangowe kijiji cha Buhekela kata ya Igoweko tarafa ya Simbo wilayani Igunga kwa tuhuma ya kusababisha kifo cha Nyandu Ndege (19), mkazi wa kitongoji cha Mwangowe wakati akimtibu nyumbani kwake.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika wilaya hiyo, John Mwaipopo amethibitisha kutokea kwa kifo cha kijana huyo alipokuwa akitibiwa na daktari feki.

Mwaipopo alisema tukio hilo lilitokea juzi saa tatu asubuhi na alipokea taarifa kutoka kwa raia mwema ambaye hakumtaja jina lake ambaye alimjulisha kuwa kuna daktari feki alikuwa akimtibu mgonjwa nyumbani kwake na amefariki dunia.

Alibainisha kuwa baada ya taarifa hiyo aliagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na baadhi ya madaktari walikwenda hadi eneo la tukio ambapo walikuta daktari feki huyo ametoroka na mke wake kwenda kusikojulikana.

Aliongeza kuwa baada ya kufanya upekuzi kwenye nyumba zake ulioongozwa na Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Tarafa ya Simbo Magengeli Ntinginya walikuta dawa aina mbalimbali na mabomba ya sindano yaliyotumika na ambayo hayajatumika yakiwa yamehifadhiwa kwenye maboksi huku mengine yakiwa yametupwa hovyo nyuma ya nyumba zake anazoishi.

Kutokana na tukio hilo la kusikitisha Mwaipopo alisema kuwa daktari huyo feki watamsaka popote alipo ili wamfikishe kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazomkabili.

Aidha Mwaipopo aliwataka wale wote wanaohitaji kuendesha zahanati wawe wamepitia mafunzo ya utabibu pia wawe na vibali kutoka mamlaka husika na kuongeza kuwa msako unaendelea kwa wilaya yote ya kuwasaka madaktari feki.

Naye mama mzazi wa marehemu Ndege, Staa Nyandu alisema mwanawe alikuwa na homa ya kawaida na walipompeleka kwenye zahanati ya serikali walikuta madaktari wote hawapo huku milango ikiwa imefungwa na waliamua kwenda kwa daktari huyo ambaye walikuwa hawajui kama hana utaalamu wowote wa udaktari.

Alisema baada ya kufika hapo mwanawe aliwekewa dripu tatu za maji ambapo alianza kutapika rangi ya njano huku akikimbia hovyo na baadaye alianza kutapika damu na asubuhi saa tatu alifariki dunia na walimzika saa 10 jioni huku akidai daktari huyo hakufika msibani na aliamua kutoroka.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho akiwemo Sophia Nyaga, Salima Emmanuel na Leonard Mabula walisema daktari huyo amefanya kazi kwa zaidi ya miaka sita na watu wengi wamekuwa wakitibiwa hapo huku wengi wao wakipoteza maisha ambapo waliishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kuokoa maisha yao.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Amada Kasigwa alisema walikamata dawa mbalimbali na pia walifanikiwa kukamata cheti bandia kikiwa kimehifadhiwa ndani ambacho hakina muhuri wowote.

Pia Kasingwa alitoa mwito kwa wananchi kwenda kutibiwa kwenye zahanati na vituo vya afya vya serikali, kwa kuwa tatizo kubwa linapojitokeza watapata fursa ya kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Wilaya ya Igunga.

Itakumbukwa kuwa Aprili 5, mwaka huu Kamati ya Ulinzi na Usalama ilifanikiwa kumkamata daktari feki, Mateo Daudi Mateo (53) wa Kitongoji cha Mgongoro kata ya Igunga mjini akiwa anaendesha zahanati bubu huku akiwa hana cheti cha udaktari ambapo tayari amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga na yupo mahabusu hadi kesi yake itakapotajwa tena Aprili 29, mwaka huu. 

Loading...

No comments: