FAHAMU ATHARI KIAFYA WANAWAKE KUCHELEWA KUZAA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Saturday, April 6, 2019

FAHAMU ATHARI KIAFYA WANAWAKE KUCHELEWA KUZAA

Wataalamu wa afya wameeleza kuwa wanawake wanaosubiri muda mrefu kabla ya kupata mtoto wako hatarini kupata uvimbe kwenye uzazi ujulikanao kama fibroids.Vilevile, wameeleza kuwa wanawake wanaweza kupata saratani ya shingo ya kizazi endapo watashiriki ngono na wanaume ambao hawajafanyiwa tohara.

Wakizungumza walipokuwa wakitoa elimu ya afya katika mkutano wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), jijini Dar es Salaam, walisema wanawake wanapaswa kuwa makini na mambo hayo mawili.

Akizungumzia suala la wanaume wasiofanyiwa tohara, daktari kutoka Hospitali ya Sanitas na mratibu wa Hospitali Narayana ya India, Limbanga Fredie alisema kuna ‘ungaunga’ na bakteria wanaojificha katika sehemu za siri za wanaume wasiofanyiwa tohara.

Alisema wanaume hao wakishiriki ngono huweza kuwa chanzo cha saratani ya shingo ya kizazi baada ya unga kubaki kwenye kizazi. “Wakati ngozi inapojivuta kwenye lile tendo ungaunga au naweza kusema kitu kama ukoko huwa vinatoka na hivyo ndivyo vinaweza kuwa sababu pia ya saratani,” alisema Dk Limbanga.

Kuhusu fibroids, alisema wanawake walio katika umri wa kuzaa wasipofanya hivyo wako hatarini kupata tatizo hilo kwa sababu mwili wakati huo unakuwa katika kipindi cha mabadiliko.

“Hivyo kama hatazaa kwa wakati ulio sahihi kwake kuzaa, ni rahisi kupata uvimbe huu kwa sababu ya mabadiliko hayo,” alisema.
Alisema umri wa kuzaa ni ule wa kati ya miaka 20 hadi 40 na endapo mwanamke atazaa katika umri wa kuanzia miaka 45 na kuendelea ni rahisi kupata uvimbe huo na wakati mwingine saratani.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka hospitali ya Narayana, Rohit Ranade alisema kwa Tanzania saratani inayoathiri zaidi wanawake ni ya shingo ya kizazi, nyumba ya uzazi na maziwa.

Alisema zipo saratani zinazosababishwa na kurithi kutoka kwa baba au mama ama mazingira akitoa mfano kutofanya mazoezi au aina za vyakula. “Kwa hiyo ugonjwa wa kansa upo juu na asilimia 50 ya wagonjwa hufariki wasifanyiwa matibabu,” alisema.

Baadhi ya wanawake waliopewa mafunzo hayo walikiri kuwa aina ya maisha wanayoishi wengi ni sababu kubwa ya magonjwa mbalimbali ikiwamo kansa.

Mtangazaji wa TBC, Fatma Matulanga alisema alichelewa kuzaa kwa sababu hakutaka mtoto nje ya ndoa. “Kulingana na imani yangu na mafundisho ya Kuran nikawa napata hofu ya kuwa na mtoto nje ya ndoa na sasa nashukuru Mungu nimepata ndoa nasubiri rehema za Mungu nitazaa,” alissema Fatma.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afya (Misa) tawi la Tanzania, Salome Kitomari alisema wasichana wasiogope kuharibu maumbile yao yakiwamo matiti wakati wanapofikia umri wa kuzaa. “Unaweza kukuta mtu anasema aaah ngoja nile ujana, nitaharibu umbile langu, nitaharibu matiti yangu, labda nile ujana kidogo kabla ya kuzaa na wanasahau kuwa kuna madhara kiafya,” alisema Salome.

Ofisa habari, sera na uchechemuzi wa Tamwa, Florence Majani alisema mwili unapokuwa unapita kipindi cha kuzaa ni vizuri kufanya uamuzi huo. Awali, mwenyekiti wa Tamwa, Alakoki Mayombo alisema wametoa mafunzo ya afya ya uzazi kwa wanahabari wanawake baada ya kugundua wengi wanakumbuka zaidi kuhudumia jamii na kujisahau katika masuala ya afya.


By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz
Loading...

No comments: