MADEREVA WA VYOMBO VYA MOTO ARUSHA WAASWA KUTOTUMIA VILEVI WAWAPO BARABARANI

Mkurugenzi wa Mahusiano kwa umma wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) John Wanyancha akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kampeni ya unywaji kiistarabu iliyozinduliwa jana Mkoani hapo ambapo madereva walipatiwa makoti ya usalama barabarani (Reflectors) kwaajili ya usalama wao.

Madereva wa vyombo vya moto mkoani Arusha wameaswa kutotumia vilevi pindi wawapo barabarani wakiendesha vyombo hivyo. Hayo yamezungumzwa  ijumaa tarehe 5 April 2019 mkoani Arusha wakati Kampeni ya unywaji wa kistarabu inayoendeshwa na Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) ikizinduliwa rasmi Mkoani humo huku madereva wa vyombo vya moto wakihimizwa kuzingatia sheria za barabarani ikiwamo kutotumia vilevi wakati wa kazi. 

Kampeni hiyo maarufu kama ‘Usinywe na Kuendesha Chombo cha Moto’ imeenda sambamba na ugawaji wa makoti ya usalama (Reflectors) kwa madereva bodaboda mkoani humo ikiwa ni mkakati wa kuhimiza matumizi ya vifaa hivyo kwa usalama wa watumiaji wa barabara. 

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha (RTO) Joseph Bukombe akimvisha kizibao cha kung'aa (Reflector) mmoja wa madereva bodaboda katika stendi kuu ya mabasi jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa kampeni ya unywaji kiistarabu inayoratiiwa na Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) uliofanyika jana jijini humo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika leo katika Makao Makuu ya Traffic jijini hapa, Mkurugenzi wa Uhusiano wa SBL, John Wanyancha amesema kampeni hiyo imelenga kutoa elimu kwa wateja wake nchini ili kupunguza matukio yanayoepukika kama ajali zitokanazo na unywaji wa pombe kupindukia. 

“Pombe isipotumika kiistarabu inaweza kuleta madhara katika jamii na mojawapo ya madhara ni pale mtu anapokunywa pombe na akaendesha chombo cha moto ikasababisha ajali jambo ambalo ni hatari kwa madereva na pia ni hasara kwa Taifa,” alisema 

Kampeni hiyo inashirikisha wadau mbalimbali ikiwamo Jeshi la Polisi-Kikosi cha usalama barabarani, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), madereva bodaboda pamoja na jamii kwa ujumla ikilenga katika kupunguza ajali zitokanazo na ulevi wa kupindukia nchini. 

Kwa upande wake,Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha (RTO) Joseph Bukombe alisema kampeni hiyo itasaidia katika kupunguza ajali zinazosababishwa na ulevi huku akiwataka madereva kuzingatia kuacha kutumia vilevi ili kujihakikishia usalama wawapo barabarani. 

“Unywaji wa pombe kiistarabu ni suala la muhimu sana kwa madereva kwasababu madereva wakiwa kwenye hali ya ulevi ni moja ya chanzo cha ajali za barabarani hivyo tunaipa kipaumbele kampeni hii hapa mkoani Arusha na tutaendelea kutilia mkazo suala hili,” alisema 

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha (RTO) Joseph Bukombe akizungumza na madereva bodaboda mkoani Arusha wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya unywaji kiistarabu inayoratibiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL).

Aliipongeza SBL kwa kuona umuhimu wa kuwalinda watumiaji wa barabara kwa kutoa elimu hiyo kwa madereva na umma kwa ujumla. 

“Pamoja na kuwa wao (Serengeti) ni watengenezaji wa pombe lakini wameona wajibu wao wa kumlinda na kuleta usalama wa madereva na watumiaji wengine wa barabara,” alisema 

Kwa mujibu wa ripoti za Jeshi la Polisi-Kikosi cha Usalama barabarani kwa mwaka 2018, jumla ya ajali 876 za bodaboda ziliripotiwa kutokea na kusababisha vifo 366 na majeruhi 694. Ripoti zinaonyesha kupungua kwa ajali hizo ambapo kwa mwaka 2017 zilikuwa 1,459 zilizosababisha vifo 728. 

Post a Comment

0 Comments