MAGUFULI AMTUMBUA NA KUMREJESHA OCD

Rais John Magufuli amemtumbua OCD wa Njombe wakati wa hotuba yake kutokana na uzembe uliosababisha mauaji ya watoto saba mkoani humo na kumrejesha katika nafasi yake dakika saba baadaye.
JPM alimrejesha OCD huyo katika nafasi yake baada ya sala ya toba, iliyofanywa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

Akizungumza leo Aprili 10, Rais Magufuli amesema sakata la maamuzi kuhusu mauaji ya watoto mkoani humo halikutakiwa lichukue muda mrefu.

“Ndiyo maana RPC nimemtoa alishindwa kusimamia hii kazi, ninataka mambo yatendeke haraka anapotea wa kwanza mpaka anafikia saba umekaa kimya. 

Ni lazima watu tuchukue hatua haiwezekani tunaleta polisi kutoka Dar es Salaam aje kusimamia hapa wewe upo haiwezekani.

“Hivi OCD wa hapa bado yupo, aondoke naye kuanzia leo siyo OCD hapa ni lazima watu tufike mahali tuwajibike, kinamama wameumia.”

Amesema mkoa wa Njombe umepata doa kubwa na kutoa angalizo,

 “Siku nyingine ataondoka mkuu wa mkoa, RAS, mkuu wa wilaya, mkurugenzi, DAS, ofisa tarafa, mwenyekiti wa kijiji wote, mpaka katibu wa CCM na wengine wote mnaondoka ili ifike mahali tuwe tunachukua hatua haraka, watani zangu Wabena na Wakinga hauwezi kutajirika kwa kuua mtoto.”

Baada ya hotuba hiyo Rais alimuomba kiongozi wa dini kuongoza sala ya toba kuhusu mauaji hayo yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka huu mkoani humo.

“Kwa hii sala OCD nimemsamehe abaki hapa hapa, mwambieni kupitia maombi haya nimewasamehe, lakini nitaomba kutoa rambirambi yangu katika hizo familia nitatoa Sh5 milioni mkuu wa mkoa ataziwasilisha kwa familia hizo,” amesema. 

Chanzo:Mwananchi

Post a Comment

0 Comments