MAJAMBAZI WACHOMOA MASHINE YA ATM UKUTANI - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, April 2, 2019

MAJAMBAZI WACHOMOA MASHINE YA ATM UKUTANI

Majambazi wamenyofoa na kutokomea na mashine ya kielektroniki ya kutolea pesa nchini Ireland ya Kaskazini.

Tingatinga la wizi limetumika kunyofoa mashine ya ATM
Majambazi hao walitumia tingatinga ambalo pia waliliiba katika kunyofoa ATM hiyo kutoka kwenye ukuta wa duka moja katika Kaunti ya Antrim.

Tukio hilo limetokea saa tisa ya usiku wa Jumatatu. Polisi wamethibitisha kuwa jengo hilo limeharibiwa vibaya.
Mmiliki wa duka hilo Walter Millar amesema kuwa ATM hiyo "itakumbukwa sana" na jamii ya eneo hilo na sasa kuna "hofu" juu ya kupatiwa mashine nyengine baada ya wizi huo.

Awali alipopokea taarifa juu ya wizi huo, mmiliki wa duka hilo bwana Millar alidhani ni uzushi tu wa Siku ya Wajinga, Aprili mosi.
"Nachoweza kusema ni kuwa, wametumia tingatinga ambalo waliliiba kwenye eneo moja la ujenzi mwishoni mwa mtaa, wakainyofoa mashine na kuipakia kwenye gari na kuondoka nayo," amesema.

"Ukuta wa jikoni umeharibiwa kabisa...tumekuwa na wakati mgumu, na ukijumlisha na hali ya kiuchumi iliyopo, vitu kama hivi vinatumaliza kabisa."

"Tulipokea simu kuhusu tukio hilo mishale ya saa 9:25 usiku kuwa tingatinga linaungua moto nje ya duka ambalo ATM imechomolewa," Inspekta wa Polisi Richard Thornton amesema.

"ATM imenyofolewa ukutani na kuharibu jengo ilipokuwa imewekwa...tunawataka mashuhuda wajitokeze, hususan walioiona gari ya rangi ya fedha."

Mwezi uliopita, polisi walitangaza kuundwa kwa kikosi kipya cha kupambana na wizi wa mashine za ATM.
Toka ulipoanza mwaka 2019, mashine saba za ATM zimeibiwa. Polisi pia wanaamini kuna makundi kadhaa ya majambazi ambayo yanajihusisha na wizi wa mashine hizo.

BBC Swahili

Loading...

No comments: