MCHUNGAJI ANASWA NA ‘UNGA’ KILO 15 DAR - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Wednesday, April 24, 2019

MCHUNGAJI ANASWA NA ‘UNGA’ KILO 15 DAR

Jeshi la Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (Adu), limewakamata raia watatu wa kigeni akiwamo raia wa Nigeria anayejiita mchungaji.

Mkuu wa kitengo cha kuzuia Dawa za kulevya nchini, ACP Salim  Kabaleke  akizungumza na waandishi  wa habari jana kuhusu watuhumiwa waliokamatwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam juzi.  Picha na Omar FungoMchungaji huyo Henry Ozoemena Ugwuanyi (44), anadaiwa kunaswa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo15 katika nyumba iliyopo Mtaa wa Pemba, Kariakoo.

Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya cha Polisi Tanzania, Alhaj Kabaleke Salim aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni raia wa Latvia, Martins Janis Plavin (20) na raia wa Nigeria, Onyebuchi Ernest Ogbu (34) anayedaiwa kuwa ndiye ‘mtaalamu wao wa kujua dawa za kulevya’ miongoni mwa genge hilo.

Salim alisema kukamatwa kwa mchungaji Ugwuanyi kunatokana na taarifa walizopewa na raia mwingine wa Lativia, Linda Mazule ambaye alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Aprili 17 akiwa na kilo 5.091 za heroin. Linda alimtaja mchungaji huyo kuwa ndiye aliyempa dawa hizo azisafirishe kwenda Poland.

Alisema kitengo cha Adu kilipoendelea kumuhoji Linda aliwaeleza kuwa alikuja nchini Aprili 11 mwaka huu akiwa na mpenzi wake ambaye na yeye ni raia wa Lativia, Plavin aliyekuwa anatarajia kusafiri na dawa za kulevya Aprili 20 mwaka huu kwenda Poland.

“Baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo tulipata taarifa za siri za watuhumiwa wengine ambao walikuwa wakishirikiana kuuza na kusambaza dawa za kulevya hizo kuwa wapo jijini Dar es Salaam,” alisema Salim.

Salim alisema Adu ilifanya operesheni katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake ili kuwabaini wauzaji na wasambazaji hao kwa ushirikiano na vyombo vingine vya dola na taasisi za kiserikali zenye mamlaka ya kisheria.

Alisema Aprili 21 saa 6 usiku, mkuu wa kitengo hicho alipokea taarifa kuwa watuhumiwa hao walikuwa maeneo ya Msimbazi Kariakoo na walipofanya msako walifanikiwa kumkamata Plavin.

Katika uchunguzi wao walibaini Plavin aliingia nchini pamoja na Linda aliyekamatwa Uwanja wa JNIA Aprili 17, na kuwa walikuwa wamepanga chumba kimoja katika hoteli mmoja (jina tunalo) iliyopo Kariakoo.

Salim alisema baada ya kuhojiwa Plavin alikiri kujihusisha na biashara haramu hiyo kwa kushirikiana na raia wawili wa Nigeria Ugwuanyi na Ogbu ambao walikuwa wamepanga nyumba namba tisa ghorofa ya nne katika mtaa wa Pemba uliopo Kariakoo.

Alisema Plavin aliwapeleka hadi kwa anayejiita Mchungaji Ugwuanyi na walipomkuta aliwapeleka hadi eneo alikopanga nyumba Mtaa wa Pemba na kuwaonyesha chumba alichokuwa akiishi.

Salim alisema baada ya kuingia ndani ya chumba chake walimkuta Mnigeria Ogbu, ambaye alikuwa mtaalamu wao wa kutambua dawa za kulevya.

Baada ya kufanya upekuzi katika nyumba hiyo watuhumiwa walikutwa na kiroba kilichojazwa mchele ndani yake kukiwa na pakiti 15 za heroin zenye uzito wa kilo 15.

“Tulipowahoji Ugwuanyi alidai yeye ni mchungaji na hata gari lake kaliandika mchungaji na Ogbu yeye ni mtaalamu na kazi yake ni kujua kama ni dawa za kulevya na kama siyo anasema na anatambua ni aina gani ya dawa za kulevya hizo,” alisema Salim.

Salim alisema baada ya kuhojiwa Ugwuanyi alidai kuwa yeye yupo nchini tangu mwaka 2017 akiwa kama mchungaji na pia akijihusisha na biashara hiyo.

Watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya upelelezi kukamilika.

Jeshi la polisi limewataka Watanzania kuwa na uzalendo na nchi yao na kuwa makini na wageni wanaopanga katika nyumba zao.
Loading...

No comments: