MMOJA AFARIKI, SITA WAJERUHIWA KATIKA MAPIGANO YA ARDHI MONDULI - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, April 1, 2019

MMOJA AFARIKI, SITA WAJERUHIWA KATIKA MAPIGANO YA ARDHI MONDULI


Watu sita wamejeruhiwa vibaya kwa silaha za jadi huku mmoja wao akifariki baada ya kuibuka mapigano ya kugombea ardhi kati ya vijiji viwili vilivyopo wilayani Monduli mkoani Arusha.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, James Manyama alimtaja marehemu kuwa ni Simeli Oltialulu mkazi wa kijiji cha Lendikinya wilayani Monduli

Mgogoro huo umekuwapo muda mrefu ukihusisha vijiji vitatu vya Lendikinya, Emairete na Arkalia ambapo wananchi wa vijiji hivyo wanagombea mipaka kati ya msitu wa hifadhi ya Lendikinya ingawa kwa sasa mgogoro huo unahusisha vijiji viwili vya Lendikinya na Emairete.

Akizungumzia tukio hilo jana usiku Jumamosi Machi 30, 2019, daktari wa zamu katika hospitali ya wilaya Monduli, Debora Karega alisema Machi 28,2019 alipokea majeruhi sita katika hospitali hiyo.

Alisema kati ya hao mmoja ameruhusiwa na wengine wawili wamehamishiwa hospitali ya mkoa Arusha ya Mount Meru kwa kuwa hali zao ni mbaya.

"Ni kweli tumepokea majeruhi sita wakiwa na majeraha mbalimbali katika sehemu za kichwani, mikononi na miguuni kutokana na kupigwa kwa sime, mishale na fimbo.”
“Wawili hali zao si nzuri, tumewahamisha kwa ajili ya kwenda kuchekiwa zaidi katika hospitali ya mkoa kutokana na kuumia zaidi maeneo ya kichwani," alisema Karega.

Mmoja wa majeruhi waliolazwa hospitali ya wilaya ya Monduli, Tingidosoto Sima (60) kutoka kijiji cha Lendikinya kata ya Sepeko alisema akiwa na wazee wenzake walikwenda eneo hilo kuzungumza na wananchi hao wa vijiji hivyo vya Lendikinya na Emairete.

Alisema walishangaa kuona wanaanza kushambuliwa na wananchi wa kijiji Emairete bila hata kuelewa sababu za kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa kamanda Manyama, vurugu hizo ziliwahi kutokea mara ya kwanza, kamati ya ulinzi na usalama ilisuluhisha na hii ni mara ya pili kutokea tena na uchunguzi ukikamilika wahusika watafikishwa mahakamani.


Loading...

No comments: