RAIS MAGUFULI KUANZA ZIARA YA SIKU MBILI MKOANI MTWARA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, April 1, 2019

RAIS MAGUFULI KUANZA ZIARA YA SIKU MBILI MKOANI MTWARA


RAIS John Magufuli atakuwa na ziara ya kikazi mkoani Mtwara wiki ijayo, ambayo itahusisha uzinduzi pamoja na uwekaji na mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ya maendeleo mkoani hapa. 

Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa wakati alipowasilisha taarifa hiyo kwa waandishi wa habari mkoani hapa kuhusu ujio huo wa Rais Magufuli, Aprili 2 hadi Aprili 4, mwaka huu. 

Kwa mujibu wa Byakanwa, miradi hiyo ni mikubwa ambayo itaenda kuchochea uchumi mkubwa kwa mkoa huu kupitia miradi hiyo na kisha kuleta tija kwa maendeleo ya mkoa huo na Taifa kwa ujumla. 

Byakanwa alisema kwamba Aprili 2, mwaka huu, Rais Magufuli anatarajia kufungua na kuweka mawe ya msingi ikiwemo kwenye Uwanja wa Ndege wa Mtwara, ujenzi wa barabara ya Mtwara hadi Mnivata na kiwanda cha kubangua korosho cha Yalin mkoani hapa. 

Aidha, alisema Aprili 3, mwaka huu, kiongozi huyo wa nchi ataweka jiwe la msingi kwenye uboreshaji wa miundombinu ya Chuo cha Ualimu Kitangali wilayani Newala. Pia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mbonde wilayani Masasi pamoja na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wilayani humo. Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, Aprili 4, mwaka huu, atafanya uzinduzi wa mradi wa barabara ya Mangaka hadi Nakapanya kuelekea Tunduru na Mangaka hadi Mtambaswala. 

Mkuu huyo wa mkoa amewaomba wananchi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kwenye mapokezi kwani ujio huo wa Rais Magufuli ni moja ya upendeleo kwa wana-Mtwara. “Ujio huu wa Mheshimiwa Rais Magufuli ni fursa na upendeleo mkubwa kwa mkoa wetu na wana-Mtwara kwa jumla kwani hii ni mara ya pili Mheshimiwa Rais kutembelea mkoa wetu wa Mtwara,” alisema Byakanwa

CHANZO: JAMIIFORUMS
Loading...

No comments: