RAIS MAGUFULI:WALIOFILISI BENKI WASAKWE

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaagiza viongozi wa mkoa Ruvuma na kamati ya ulinzi na usalama mkoa huo kufuatilia na kuwabaini watu waliosababisha Mbinga Community Bank kufilisika na kusababisha kero kwa wakulima wa wilaya hiyo wakiwemo wa kahawa.

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Ametoa agizo hilo jana Jumapili Aprili 7, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa Mbinga mkoani Ruvuma baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mbinga hadi Mbambabay yenye urefu wa kilomita 67 na thamani ya Sh134.712bilioni.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda kueleza kumekuwa na changamoto mbalimbali katika vyama vya msingi hasa kwa wakulima waliopeleka kahawa nyingi kulipwa fedha kidogo lakini wanaopeleka kidogo kulipwa fedha nyingi.

Akitoa maagizo, Rais Magufuli amesema mbunge wa jimbo hilo, mkuu wa wilaya na mkoa wafuatilie kwa kushirikiana na vyombo vya dola ili wampate aliyefilisi benki hiyo ili kukata mzizi wa fitina.

Amesema wapo watu wamekuwa wakipata utajiri na kutamba kwa kujinufaisha na fedha za watu wanyonge na maskini bila kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.

Kiongozi huyo ameonya kwenye awamu ya uongozi wake hatakubali vitu vya ovyoovyo vilivyokua vikifanywa na baadhi ya watu wachache wanaojiita matajiri kwa kuwanyonya wananchi wachache viendelee.

"Viongozi wachukue hatua na waache unafiki wa kusubiri hadi mimi nifike ndipo mnitajie kero ili nizifanyie kazi wakati nyinyi mpo hapa na wanaowadhulumu wakulima mnawajua,” amesema.

“Pia Mbunge unanitaka nichukue hatua kwa watu ambao wamedhulumu wakulima wakati nawe upo hapa, kwa nini usingechukua hatua au kunipa majina yao au kuwataja hadharani,” amehoji

“Na waliofilisi benki mnawajua na hajawachukulia hatua yoyote wapo hapohapo na waliowadhulumu wakulima wanawajua, ungenitajia hayo majina au ungenikabidhi hapa uone ambacho ningewafanya,’’ amesema

Ameendelea kuzungumzia benki hiyo akisema, “Nafahamu miaka ya nyuma kulikuwa na benki hapa, lakini naambiwa walioimaliza ni watu wa hapa. Muda mwingine matatizo ya kumaliza hapa tunasubiri hadi kiongozi mkubwa aje.”

“Nimezungumza haya ili tutafute mzizi wa fitina, tukifunika funika hatutafika sababu kuna watu wamefanya mambo ya ajabu huku wakitembea vifua mbele kwa utajiri wa mali za maskini waliowadhulumu,” amesema.

Rais Magufuli amesema alitegemea Mapunda amkabidhi orodha ya watu waliokuwa wanahusika na kununua kahawa na kuwadhulumu wananchi kuwa ni fulani na fulani, badala yake anaficha na kuyafumbia.

“Nataka majibu yapatikane kwa watu waliokuwa wakinunua kahawa na kuwadhulumu wakuliwa. Mapunda mchapakazi, lakini ifike mahali tuache kuogopa na kufanya unafiki ungewataja waliowadhulumu wananchi wako na ungenikabidhi majina hapa leo ungeona,” amesema Rais Magufuli.

Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

0 Comments