SAMATTA AZUIWA KUOA BABA YAKE AFUNGUKA KISA!-VIDEO - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Sunday, April 28, 2019

SAMATTA AZUIWA KUOA BABA YAKE AFUNGUKA KISA!-VIDEO
HUU ni mwendelezo wa simulizi ya baba mzazi wa mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta ajulikanaye kwa jina la Ally Samatta. Katika simulizi ya kwanza iliyotoka juzi Jumatano kwenye Gazeti la Championi Jumatano, baba Samatta alizungumzia mambo kadhaa yanayomuhusu nahodha huyo wa Taifa Stars ikiwemo alivyoanza kujifunza soka akiwa na umri wa miaka miwili.
Aliishia pale ambapo wamehamia jijini Dar es Salaam wakitokea Mbeya, baadaye baba yake huyo mzazi alikuwa akimpeleka Coco Beach kwa ajili ya kunolewa hadi alipotua Mbagala Market ambayo ilibadilishwa jina na kuitwa African Lyon. Sasa endelea…

KISA MPIRA, ASHINDA NA NJAA
“Kutokana na kuupenda sana mpira, mara nyingi alikuwa akiondoka nyumbani kwenda kucheza na hakumbuki kuja kula chakula cha mchana, kula yake ilikuwa ya shida sana, siku nyingine anakula usiku tu. “Kipindi hicho alikuwa na miaka kumi na mama yake alikuwa bado hajafariki.

ALELEWA FAMILIA YA KIASKARI
“Nidhamu aliyokuwa nayo Samatta ilitokana na malezi tuliyompa wazazi wake ambapo mimi nilikuwa askari na mama yake mzazi pia alikuwa askari, hivyo hali aliyokuwa akikutana nayo nyumbani ndiyo iliyomfanya awe na nidhamu ya hali ya juu, siyo kwake tu hadi kaka zake.

MAMA YAKE AFARIKI
“Wakati akiwa bado na umri wa miaka 10, mama yake mzazi bi Hadija Aloyce Luwongo alifariki dunia na hapo ndipo safari ya kuanza kumlea peke yangu ilipoanza. “Nakumbuka ilikuwa Julai mwaka 2000 ilikuwa ni miaka mitatu tu tangu tulivyohamia jijini Dar, ilikuwa huzuni sana kwangu kuwalea watoto peke yangu bila ya mama yao mzazi. “Ilipofika mwaka 2003, nilioa mke mwingine anayeitwa Ashura Shomvi, nikakaa naye miaka sita, huyo alikuwa wa kwanza kumlea Samatta akiwa kijana mdogo, nikafanikiwa kuzaa naye mtoto mmoja wa kike ambaye ndiye mtoto wa kike pekee kwangu.

“Niliachana naye baada ya kuwa naye kwa miaka sita, nikaoa mwanamke mwingine anayeitwa Amina Swalehe, alikuwa Mngoni kutoka Songea, naye nilikaa naye mwaka mmoja tu akaniacha akaondoka. “Baada ya hapo ilipofika mwaka 2011, nilifanikiwa kumuoa mke mwingine anayeitwa Khadija Omary ambaye ndiye ninaye hadi sasa, huyu alimkuta Samatta tayari ameshakuwa mkubwa na anaendelea kucheza mpira.


ANYIMWA CHAKULA
“Wakati nilipokuwa na mke wa pili Ashura baada ya mama yake Samatta kufariki, nilikuwa nikipata malalamiko kutoka kwa Mbwana na kaka yake Mohammed kwamba walikuwa wananyimwa chakula. “Alikuwa akichelewa kupika chakula kwa makusudi, hivyo watoto wakawa wanakwenda kucheza mpira bila ya kula.

“Alitegea watoto wameenda kucheza ndiyo anapika, muda ambao alikuwa akipika ilikuwa saa 10 kwa madai alikuwa akinisubiria mimi nirudi ndiyo apike tule pamoja, kitendo hicho sikuwa nimekipenda. “Muda wa watoto kula chakula ilikuwa saa saba lakini alikuwa hafanyi hivyo, akasababisha wawe wanaondoka bila ya kula, walikuwa wakinilalamikia sana kuhusu suala hilo, ikabidi nifuatilie.

AANZA KUJIPIKIA KWA KISIRI
“Baada ya kuona hali hiyo inaendelea kila siku, yeye na kaka yake wakaamua kununua jiko na unga, wakaanza kujipikia ndani kisirisiri, kisha wanakwenda kucheza mpirani, mama yao alikuwa hajui. “Hali hiyo iliendelea kwa muda pasipo mimi kujua kinachoendelea nyumbani, baadaye baada ya mimi kugundua nilimlaumu sana mama yao kutokana na kitendo hicho alichokuwa akikifanya, ilikuwa ni vyema kuwapikia watoto kisha mimi akaniwekea.

“Wakati wanafanyiwa mambo hayo walikuwa wakicheza mpira wa ndondo sehemu mbalimbali, baada ya kuondoka yeye, wake wengine niliowaoa hawakuwa na shida yoyote kwa kuwa na wao walikuwa tayari wameshakuwa wakubwa
hivyo walikuwa wakijua nini cha kufanya.

AKOSA SAPOTI KUTOKA KWA MAMA ZAKE
“Wakati mama yake mzazi yupo hai alikuwa akipata sapoti kubwa kutoka kwake katika kucheza mpira, lakini baada ya kupata wake wengine hawakuwa wakimpa sapoti inayostahili na badala yake sapoti kubwa ya kucheza mpira alikuwa akiipata kutoka kwa kaka zake. “Kaka zake ni watu wa mpira hivyo walikuwa wakimsaidia sana hadi hapo alipofikia kwa kuwa na wao walikuwa wakiupenda licha ya kushindwa kufanikiwa kusonga mbele.

AKATAA SHULE
“Watoto wangu wote wamekataa kuendelea na elimu ya kidato cha tano, wote wameishia kidato cha nne akiwemo Samatta. “Niliwaambia uwezo wa kuwaendeleza kimasomo ninao baada ya kumaliza kidato cha nne, lakini hawakutaka kuendelea japokuwa hawakufeli, walikuwa wanapendelea mpira zaidi, sijui walikuwa wanataka kuyaingilia maisha haraka. Usikose kufuatilia Championi Jumamosi kufahamu baada ya kukataa kujiunga na kidato cha tano, ilikuwaje.
MAKALA NA KHADIJA MNGWAI – CHAMPIONI IJUMAA, APRILI 26, 2019
Loading...

No comments: