SOKWE MTU WAPIGA 'SELFIE' DR CONGO - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, April 23, 2019

SOKWE MTU WAPIGA 'SELFIE' DR CONGO

Sokwe mtu wawili wameshangaza wengi kwa kuweza kuiga mkao wa binaadamu waliponaswa kwenye picha iliyopigwa kwa kutumia kamera ya mbele ya simu ya mkononi, maarufu kwa lugha ya mtandaoni kama selfie.

Mathieu Shamavu na Sokwe
Sokwe hao wamepiga selfie hiyo na askari wa wanyamapori ambao waliwaokowa kutoka kwenye makucha ya majangili walipokuwa wadogo.

Picha hiyo imepigwa katika makao ya sokwe yatima kwenye Hifadhi ya Taifa ya Virunga nchini DR Congo, ambapo sokwe hao wamekuwa wakilelewa toka wazazi wao kuuawa na majangili.

Naibu mkurugenzi wa hifadhi hiyo Innocent Mburanumwe ameiambia BBC kuwa sokwe hao walijifunza kuiga tabia za binaadamu wanaowatunza toka walipokuwa wadogo.

Mburanumwe pia ameiambia BBC kuwa mama wa sokwe hao waliuawa Julai 2017.

Sokwe hao waliokolewa wakiwa na umri kati ya miezi miwili na minne.

Muda mfupi baada ya wazazi wao kuuawa, sokwe hao waliokolewa na askari na kutunzwa kwenye makazi maalumu ndani ya hifadhi ya Virunga mpaka hii leo.

Kwakuwa wamekuwa wakiwa na askari waliowaokoa, Mburanumwe anasema, "wanaigiza tabia za binaadamu" - na kusimama kwa miguu miwili ndio namna yao ya "kujifunza kuwa binaadamu".

Hata hivyo "haitokei kila wakati", amesema Mburanumwe.

"Nilipigwa na mshangao nilipoiona picha hiyo .... ni picha ichekeshayo. Ni jambo la kushangaza kuona namna gani sokwe wanaweza kuiga mwanadamu na kusimama."

Kuwa askari wa wanyama pori kwenye eneo hilo hata hivyo si kazi nyepesi au ya raha tele - ni kazi ngumu sana.
Loading...

No comments: