TANZANIA NA MISRI ZARIDHIA UJENZI WA KIWANDA CHA KUCHAKATA NYAMA HAPA NCHINI. - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, April 1, 2019

TANZANIA NA MISRI ZARIDHIA UJENZI WA KIWANDA CHA KUCHAKATA NYAMA HAPA NCHINI.


Tanzania na Misri zimeweka historia nyingine ya ushirikiano baada ya kutia saini hati ya makubaliano ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuchakata nyama na mazao mengine ya mifugo kinachotarajiwa kutoa ajira kwa takribani watu 5,000.

Imeelezwa kuwa kiwanda hicho kitakajengwa kwa ubia baina ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) ya Tanzania na Kampuni ya Necai ya Misri na baada ya ujenzi wake kukamilika, kitazalisha nyama na bidhaa za ngozi kama viatu, mikanda, mabegi na chakula cha mifugo.

Kiwanda hicho kitakachoitwa Ruvu Integrated Industry kikiwa na uwezo wa kuchinja ng'ombe 1,500 na mbuzi 4,500 kwa siku, kitajengwa katika Ranchi ya Ruvu wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano hayo baina ya nchi hizo jijini Dar es Salaam juzi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alisema ujio wa kiwanda hicho ni faraja kubwa kwa wafugaji hasa katika kipindi hiki ambacho hawana masoko ya uhakika ya mifugo yao.

Waziri Mpina alisema ujenzi wa kiwanda hicho pia kunapeleka salamu njema kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Maendeleo Mashariki mwa Afrika (IGAD) na mataifa mengine ambayo yanategemea mazao ya mifugo kutoka Tanzania.

Alisema asilimia 1.4 ya mifugo yote duniani iko Tanzania na asilimia 11 ya mifugo yote Afrika iko Tanzania, hivyo kuna uhakika wa viwanda hivyo vinavyoanzishwa sasa kupata malighafi ya kutosha muda wote.

Aliihakikishia Misri kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika uzalishaji wa mifugo pamoja na huduma za mifugo ili kuhakikisha malighafi hiyo ya viwanda inakuwa bora na inapatikana wakati wote.

Waziri Mpina aliagiza timu ya wataalamu kutoka Tanzania na Misri kukamilisha haraka upembuzi yakinifu wa mradi huo ili ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa, mkataba rasmi wa ubia wa ujenzi na uendeshaji wa kiwanda hicho uwe umesainiwa.

Pia aliwaagiza watendaji wote wa serikali wanaoshiriki katika majadiliano hayo kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha mkataba huo kutiwa saini.

Watendaji wanaohusika ni wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi nyingine zitakazohusika na mchakato wa upembuzi yakinifu.

Mbali na hilo, Waziri Mpina pia aliiomba Serikali ya Misri kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine ya mifugo na uvuvi kwa kuwa fursa bado ni nyingi hasa katika uendeshaji wa Shirika la Uvuvi Tanzania (Tafico) ambalo serikali tayari imeshalifufua.

Waziri huyo alisema fursa za uvuvi wa ukanda wa uchumi wa Bahari Kuu (EEZ) ni kubwa kwa Tanzania kwa kuwa ina eneo la kilomita za mraba 223,000, ukanda huo ukiwa unafaa kwa uvuvi wa samaki aina ya jodari na wengine ambao ni wa daraja la kwanza duniani.

Aliiomba Misri kuwekeza katika viwanda vya kuchakata samaki wa bahari na maji baridi, ufugaji wa samaki pamoja na kununua meli kubwa za uvuvi zitazovua katika maji ya ukanda wa uchumi wa bahari kuu.

Balozi wa Misri, Mohamed Gaber Abulwafa, alisema hatua ya utiaji saini hati ya makubaliano hayo ni kielelezo cha ushirikiano uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 baina ya Misri na Tanzania katika kuchochea uchumi wa mataifa hayo mawili.

Alisema Misri imevutika kuwekeza kwenye sekta hiyo ya mifugo baada ya kubaini Tanzania inayo mifugo mingi na bora na ujio wa mradi huo ni matokeo ya mazungumzo ya awali baina ya Rais John Magufuli na Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi, alipotembelea nchini mwaka 2017.
Loading...

No comments: