WASIOJULIKANA WAVAMIA OFISI YA TRA SHINYANGA, WAIBA NYARAKA, LAPTOP NA PESA


Watu wasiojulikana ambao idadi yao haijulikani wamevamia ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa kodi wa Kahama, Shinyanga na kuondoka na kompyuta mpakato moja na baadhi ya nyaraka za kodi pamoja na Sh2 milioni baada ya kuwafunga kamba walinzi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Richard Abwao alisema jana kuwa watu hao walivamia ofisi hizo usiku wa kuamkia jana na kwamba uchunguzi unaendelea kubaini waliohusika na sababu za kufanya hivyo kama ni kuiba fedha au nyaraka za ofisi.

Alisema watu hao baada ya kuwafunga kamba walinzi walivunja dirisha la nyuma na kisha kuingia ndani na kupora vitu hivyo na kwamba kwa sasa walinzi hao wanashikiliwa pamoja na baadhi ya maofisa wa mamlaka hiyo ili kusaidia uchunguzi wa polisi.

Naye kaimu meneja wa TRA mkoa wa mamlaka hiyo Kahama, Michael Nsobi alisema wezi hao baada ya kuingia ndani walivunja milango mitatu na kuingia sehemu ilikohifadhiwa selfu ya kutunzia fedha na kuchukua Sh2 milioni zilizokuwa za matumizi ya ofisi.

Alisema hata hivyo bado wanafanya uchunguzi kubaini kama kuna vitu vingine zaidi vilivyoibiwa ndani ya ofisi hizo zaidi ya fedha hizo, kompyuta mpakato moja na nyaraka za walipa kodi.

Aidha, Nsobi alisema wezi hao wamefanya uharibifu kwa kuvunja vunja milango na madirisha wakati wa kuingia ndani na kwamba walinzi walinzi wawili waliokuwa wakilinda ofisi hizo wakiwa na bunduki walifungwa kamba bila kuporwa silaha zao na polisi waliondoka nao kwa ajili ya kuwahoji.

Mmoja wa wananchi wa Kahama ambaye ni mfanyabiashara, Jumanne Lucas alisema wizi huo una mashaka kutokana na kwamba hakuna mfanyabiashara anayekwenda kulipa kwa fedha taslimu katika ofisi hiyo bali kupitia benki, hivyo huenda wezi hao lengo lao lilikuwa ni nyaraka kwa ajili ya kuficha jambo fulani.

Post a Comment

0 Comments