Amwagiwa mafuta ya taa na kupigwa kiberiti ili kuondoa mapepo - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Wednesday, May 1, 2019

Amwagiwa mafuta ya taa na kupigwa kiberiti ili kuondoa mapepo


Serengeti. Ni kama hadithi, lakini ndiyo ukweli. Phillipo Elias, mkazi wa kijiji cha Musati wilayani hapa, ameuguzwa moto mwilini wakati akiombewa kanisani ili aponywe maumivu ya kichwa.

Elias (22), ambaye anafanya kazi ya kuchunga mifugo kijijini hapo akitokea Kakonko, Kigoma, alisema jana akiwa katika Hospitali Teule ya Nyerere, Serengeti kuwa alimwagiwa mafuta ya taa na kupigwa kiberiti kama njia ya kumfanyia ibada ya kumtoa pepo.


Kwa mujibu wa maelezo yake, tukio hilo lililotokea juzi, lilifanywa na mchungaji wa Kanisa la Cag Calvary, Anna Butake.

Hata hivyo, mchungaji Anna amekana kumchoma moto muumini huyo akisema hajui kilichotokea hadi Phillipo akaungua kwa sababu yeye alilenga kuchoma moto nguo zilizoonekana kuwa na zindiko.

“Ilipofika zamu yake (Phillipo) alitoa nguo ya ndani iliyokuwa na nembo ya mauaji, ndipo nikamwambia aishikilie tuichome moto. Sijui kilichotokea hadi naye akaanza kuungua moto,” alisema mchungaji huyo akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.

Awali, akizungumza akiwa wodi ya wanaume katika hospitali hiyo, Philipo alisema alikwenda kwa mchungaji huyo kwa ajili ya maombi kutokana na kumfahamu akidai wanatoka wote Kigoma.

“Mimi na mchungaji Anna tunatoka wote mkoa wa Kigoma na niliamua kwenda kwake badala ya kanisa langu la Pefa ninakoabudu kutokana na taarifa kuwa ana nguvu za uponyaji,” alisema Phillipo.

“Nilipofika niliamriwa kupiga magoti huku nimefunga macho, nikamwagiwa mafuta ya taa kwa lengo la kuchoma nguo zangu alizosema zina pepo.”

Akionekana mwenye kuhisi maumivu makali, alisema wakati nguo zake zinateketea alianza kupata maumivu hadi kulazimika kufungua macho na kushuhudia mchungaji na waumini wengine wakiomba bila kujali hali iliyokuwa ikimtokea.

“Nililazimika kupiga kelele kuomba msaada baada ya kuona kifo kinaninyemelea. Nashukuru Mungu nimeokolewa maana ningekufa kwa kuteketea moto.”

Mchungaji

Mchungaji Anna alisema licha ya Phillipo pia walikuwepo watu wengine wawili waliofika kwa ajili ya maombi na kusalimisha zana zao za uganga.

Alisema Phillipo alikusudia kutumia nguo ya ndani yenye nguvu za giza kumwangamiza yeye (mchungaji) kama ambavyo tayari amefanya kwa wachungaji wengine 16 mkoani Kigoma.

“Jambo la ajabu ni kwamba nguo aliyoishikilia mkononi ilipomwagiwa mafuta na kuwashwa moto, Phillipo ndiye alianza kuungua badala ya nguo. Kuona hivyo ikabidi tuongeze maombi ili kuteketeza nguvu za giza,” alisema.

Akijibu tuhuma za kuwa na nguvu za giza anazotumia kuwaangamiza wachungaji, Phillipo alikana akisisitiza alikwenda kuombewa baada ya maumivu ya kichwa ya muda mrefu.

Hata hivyo, mchungaji Anna alishangazwa na tukio hilo akisema aliagiza nguo hiyo ishikiliwe na Phillipo wakati inateketezwa kwa sababu nguvu za giza huangamizwa na kuteketezwa kwa kumpa mhusika kushikilia vifaa vyake. Alisema nguvu yake ya maombi ndiyo ilimfanya Phillipo aungue moto badala ya nguo aliyoishikilia huku akidai bila nguvu za Mungu alizonazo yeye ndiye angeteketea kwa moto.

Akizungumzia hali ya majeruhi huyo, muuguzi wa zamu katika wodi ya wanaume, John Nyang’ombe alisema inaendelea vizuri baada ya kupata matibabu.

Kaimu ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Ikengo Mwita alisema baada ya tukio hilo aliamuru walinzi wa jadi maarufu kama Sungusungu kumkamata mchungaji Anna na kumfikisha kituo cha kidogo cha Polisi cha Kenyana.

“Hata hivyo baada ya muda nilimuona akirejea nyumbani akiwa na waumini wake huku wakiimba nyimbo zao za dini,” alisema.

Mkuu wa polisi wilayani Serengeti, Methew Mgema alisema wanafuatilia na kuchunguza kwa makini tukio hilo ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheriaCHANZO;JF.
Loading...

No comments: