Dk Reginald Mengi Afariki Dunia,Rais Magufuli Atoa Salamu za Rambirambi - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, May 2, 2019

Dk Reginald Mengi Afariki Dunia,Rais Magufuli Atoa Salamu za Rambirambi

Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi amefariki dunia. Taarifa za awali ambazo zimerushwa leo asubuhi na kituo cha televisheni cha ITV imesema, "Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk Reginald Mengi amefariki dunia." 

Dk Reginald Mengi Enzi za Uhai Wake


Mfanyabiashara huyo maarufu ndani na nje ya Tanzania inaelezwa amefariki usiku wa kuamkia leo Alhamisi Mei 2, 2019 akiwa Dubai alipokuwa anapatiwa matibabu.

Rais wa Tanzania, John Magufuli ametoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi (75).

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Rais Magufuli ameandika, “Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee na rafiki yangu Dk Reginald Mengi.”

“Nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu na maono yake yaliyopo katika kitabu chake cha I Can, I Will, I Must. Poleni wanafamilia, wafanyakazi wa IPP na Jumuiya ya Wafanyabiashara,” ameandika Rais Magufuli

Pia Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kifo cha Mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi ni zaidi ya pigo kwa maelezo kuwa alikuwa ni mtu mwema kwa kujali watu wengine.

"Kwa kawaida tunasema mtu akifa ni pigo, lakini hili ni pigo kubwa na ni pigo halisi hasa ukiangalia alikua akisaidia makundi mbalimbali hasa ya walemavu na wajasiriamali.”

“Naamini watoto wake wataendeleza yale aliyokuwa akiyafanya wakati akiwa hai kwani ndio sehemu ya mafanikio yake,” amesema Mghwira.

Ameongeza, “Hata hapa mkoani kwetu alikua anatutia moyo sana akisikia tumefanya jambo jema alikua anaongezea na mawazo yake mengine ili kufanya vizuri zaidi.”

Amebainisha kuwa Mengi alikua si mtu wa kulalamika bila sababu na hata akifanya hivyo anakuwa na sababu ya msingi huku akikueleza nini cha kufanya.
Loading...

No comments: