KUTANA NA ABDALAH NYAMBI, KIJANA ANAYEBADILISHA UCHAFU WA PLASTIKI KUWA VITOFALI (PAVEMENTS) - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, May 3, 2019

KUTANA NA ABDALAH NYAMBI, KIJANA ANAYEBADILISHA UCHAFU WA PLASTIKI KUWA VITOFALI (PAVEMENTS)

Abdalah Nyambi (kushoto) akikusanya uchafu wa plastiki na wenzake. 
Utunzaji wa mazingira ni jambo linalopigiwa chapuo sana, hasa wakati huu ambapo mabadiliko ya tabia ya nchi yanavyoonekana waziwazi ingawa imekuwa changamoto sana kutokana na uelewa mdogo, na tamaduni ya kutojali utunzaji bora wa taka nchini Tanzania. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mazingira ya mwaka 2017 {National Environment Statistics Report, 2017 (NESR, 2017)}, inaonyesha kwamba Jiji la Dar lilizalisha taka tani takribani 4,600 kwa siku na inakadiriwa kuzalisha tani 12,000 kwa siku ifikapo mwaka 2025.

Data zinazoonyesha mkusanyiko wa uchafu jijini Dar es Salaam.
Dar es salaam ni miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi sana Afrika, huku likiwa na watu wapatao Milioni 4.3 kwa Sensa ya Mwaka 2012. Utunzaji bora wa taka bado ni tatizo, huku miundombinu ya kuhifadhia taka ikitajwa kuwa changamoto. Tatizo la utunzaji bora wa taka linatajwa kukumba sana makazi holela, ambapo asilimia 70-80% ya wakazi wa mijini huishi bila ya kuwa na miundombinu wezeshi ya kuhifadhi taka ipasavyo. 

Abdalah Nyambi(26), ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu Kampala (Kampala International University) shahada ya Sayansi ya Kompyuta (Computure Science). Ni kijana mwenye ndoto ya kupambana na taka za plastiki kwa kuzigeuza kuwa ‘pesa’ kupitia uzalishaji wa matofali (pavements). Yeye pamoja na wenzake 8 wameanza kuleta mabadiliko katika jamii wanayoishi huko Gongo la mboto kwa kuonyesha jinsi taka za plastiki zinavyoweza kuwa pesa. 

Mwishoni mwa Mwaka 2018, Abdalah alikutana na Liberatha Kawamala (24) katika maonyesho yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa Tanzania, ambapo bidhaa mbalimbali zikiwepo mapambo yatokanayo na chupa za plastiki yalikuwa yakionyeshwa. 

Maonyesho hayo ndiyo yaliwafanya wawili hawa kuungana na kuamua kufanya kazi pamoja ili kufikia lengo lao la kutengeneza ajira kwa vijana kupitia mapambano ya uchafuzi wa mazingira wa bidhaa za plastiki. Muungano huo umewafanya kuanzisha Kampuni yao iitwayo “Plastic recycle and youth Organizatio(PREYO)” yenye wasichana 2 na wavulana 7 ambapo wanafanya kazi kwa pamoja kutoa elimu kwa vijana juu ya utunzaji wa mazingira pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za kujipatia kipato. 

Vijana wanaounda kundi la PREYO wakiwa katika picha ya pamoja huku wameshikilia pavements wanazotengeneza. 

Wengine hufanya kazi kutokana na wito, wengine hufanya kazi kutokana na kukosa cha kufanya, lakini kwa Liberatha utunzaji wa mazingira ni wito wa moyoni ambao umemfanya kuacha taaluma yake na kupambania mazingira. 

“Nimesomea Logistics na Transpotation lakini moyo ukanipeleka kwenye mazingira; Watu wengi huniuliza kwanini umesomea logistic na haihusiani na mazingira, huwa nawajibu kama unapenda kitu flani, ni vizuri ukifanye hicho” Anasema Liberatha 

Ametumia sehemu kubwa ya muda wake kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira , ikiwemo kufungua Zaidi ya Club 300 za mazingira katika shule za Msingi jijini Dar es salaam ambapo anafundisha umuhimu wa utunzaji wa mazingira na namna ya kukabiliana na taka za plastiki. 

Watu wengi katika jamii hawana tamaduni ya kutupa taka sehemu maalumu, mara nyingi hutupa taka ovyo ovyo bila kuzingatia kanuni za utunzaji wa mazingira suala linalohatarisha usafi wa jiji hili. Ukosefu wa mifuko ya kutenganisha taka kulingana na aina zake mathalani, karatasi, chupa, na taka zinazooza hufanya hali kuwa tete Zaidi hasa kwa watu wanaofanya kazi ya ukusanyaji wa taka mitaani.

“Wale waliojiajiri kukusanya chupa za plastiki, hawapiti kila siku, hivyo ni changamoto kidogo, unafanya usafi lakini unakuta una lundo la chupa za plastiki na hujui pa kuzipeleka. Nilichukua changamoto yangu kama fursa”. Anasema Liberatha 

Kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu, na kujihusisha katika ukusanyaji wa chupa za plastiki mitaani ni jambo lisilo la kawaida nchini Tanzania, kwani baadhi ya watu huwachukulia waokota chupa za plastiki kama wendawazimu au watu walioshindwa maisha, lakini kwa Abdalah Nyambi na wenzake hilo ni tofauti kabisa. 

“Kuna wakati nilitaka kuacha kuokota makopo kabisa, wanafunzi wenzangu walinichukulia kama mwenda wazimu na walinivunja moyo” Anasema Abdalah 

Abdalah yeye anaona sio kama jamii haijali kuhusu mazingira, bali imekosa elimu bora kuhusu utunzaji wa mazingira. 

“Watu wanakosa uelewa tu. Kama tukianza kuelimisha wananchi, nafikiri wote watakuwa wanatambua kuhusu mazingira na umuhimu wa kuyatunza kwa kufanya mambo rafiki kwa mazingira” Anaongezea 

Kilometa 21 kutoka Gongo la Mboto, Liberatha anawasili katika shule ya Msingi Makumbusho tayari kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira katika Club ya “root and shouts” moja kati ya club 300 za mazingira jijini Dar es salaam anazozisimamia. 

Wanafunzi wa shule hii wana furaha kumuona Liberatha, na tayari kupokea elimu ya utunzaji wa mazingira, kwani ukweli ni kwamba watoto ni taifa la kesho, hivyo ili kuwa na taifa linalojali na kutunza mazingira, ni muhimu kutoa elimu kwa watoto wadogo ili watambue mapema umuhimu wa mazingira. 

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Makumbusho walio katika klabu ya mazingira
Siku ya Mwisho, Abdalah akiwa amevalia Kaptura yake Nyekundu, shati yake ya Chungwa pamoja na Mask kwenye pua, tayari kuzalisha matofali maalumu yanayotokana na taka za chupa za plastiki. Tofauti na siku nyingine, Siku hii kikundi cha watu tisa kipo tayari, wengine wakikusanya Chupa za plastiki, wengine wakiandaa moto na wengine wanakusanya mchanga. 

Chupa za plastiki zinamiminwa kwenye pipa, moto unachochewa, na chupa zinayeyuka taratibu lakini kwa uhakika. 

Chupa pamoja na uchafu wa plastiki vikiwekwa kwenye pipa la moto kwaajili ya kuyeyuka
“Tulianza mradi huu kwasababu tuliona tatizo la mchanga, mchanga mwingi unatumika kuzalisha aina hizi za tofali, mradi huu unatumia mchanga kidogo pamoja na chupa nyingi”. Anasema Liberatha. 

Hakika sio zoezi dogo, Moshi mzito unapanda angani, huku Abdalah akichanganya Mchanga na uji-uji wa chupa kwenye pipa, tayari kutengeneza matofali madogo (pavement). Kwa siku wana uwezo wa kuzalisha matofali 25 pekee, matofali yasiyopitisha maji, yanayotumia mchanga kidogo na plastiki nyingi, matofali imara. 

Matofali (Pavements) yaliyotengenezwa kutokana na uchafu wa plastiki 
Changamoto kubwa ya uzalishaji wa tofali hizi ni ukosefu wa mitambo ya kisasa ya uzalishaji, ambayo itaweza kuyeyusha chupa bila kutoa Moshi katika mazingira, na kufanya uzalishaji huu kuwa bora na kutunza mazingira haswaa tofauti na sasa unavyo hatarisha Afya za wazalishaji pamoja na ajamii inayo wazunguka. Matarajio ya kikundi hiki ni kupata mtambo huo na kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu taka za plastiki. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Mazingira ya Umoja wa mataifa (UNEP 2018) inatabiri ifikapo mwaka 2050 uzalishaji wa taka za plastiki duniani utafikia Tani Billioni 12, hivyo kama hakutakuwa na jitihada za maksudi za kukabiliana na taka hizi, hasa uzalishaji wa bidhaa za plastiki zinazotumika mara moja, hali ya sura ya nchi itakuwa mbaya Zaidi ya sasa. 

Ingawa jitihada za maksudi zimekuwa zikifanywa na serikali pamoja na Taasisi mbalimbali ili kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, bado baadhi ya watu hawaoni umuhimu wa wao kuwa sehemu ya utunzaji mazingira, bali huiachia serikali kama mhusika mkuu, suala ambalo sio sahihi. 

Aidha uwepo wa taasisi nyingi zinazoshuhulika na utunzaji wa mazingira, ilihali hazina ushirikiano wa pamoja, huondoa nguvu ya kukabiliana na matatizo ya mazingira kwa umoja. 

“Kuna watu wengi wanajihusisha na mazingira lakini kinachokosekana ni kitu cha kutuuunganisha pamoja, Unaweza kusikia mtu flani kwenye chombo cha habari kwamba anatengeneza matofali ya plastiki, lakini hufahamu wapi anaishi, ofisi yake ipo wapi, hakuna jukwaa la kutuunganisha pamoja ili tutunze mazingira yetu”. Anasema liberatha. 


Imeandaliwa na Goodhope Amani: 
Mwandishi wa kujitegemea anayeandika kuhusu mazingira, Ubunifu na Siasa. 
Mawasiliano: 0765969987

Loading...

No comments: