MDUDE CHADEMA ASIMULIA JINSI ALIVYOTEKWA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, May 10, 2019

MDUDE CHADEMA ASIMULIA JINSI ALIVYOTEKWA

Mwanaharakati Mdude Nyagali maarufu kwa jina la Mdude Chadema asimulia jinsi alivyotekwa na watu wasiojulikana Jumamosi iliyopita.

Kijana Mdude Nyagali maarufu kwa jina la Mdude Chadema

“Kutekwa kwangu kuna uhusiano kabisa na harakati zangu za kisiasa, ila hilo haliwezi kupunguza ari ya kuendelea na mapambano kupigania haki za wanyonge. Maisha yangu ya kawaida sana,” alisema. “Walioniteka walikuwa na Land Cruiser la Sh100milioni na mie mfukoni nina 20,000.”
Mdude ambaye alipatikana juzi usiku katika Kijiji cha Inyala, Mbeya baada ya kutekwa na watu wasiojulikana akiwa ofisini kwake Vwawa- Mbozi, alipatiwa huduma ya kwanza na wananchi waliomkuta akitambaa kando ya barabara.
Akizungumza na Mwananchi jana katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya anakopatiwa matibabu, Mdude ambaye kabla ya mahojiano alikuwa akipatiwa vipimo mbalimbali na kuhojiwa mara kadhaa na polisi waliovaa kiraia, alisema alitekwa saa 12 jioni na akiwa katika gari la watekaji, alipigwa hadi akapoteza fahamu.
Diwani wa Nsalala katika mji mdogo wa Mbalizi, Kisman Mwangomale ndiye aliyetoa taarifa za kupatikana kwa Mdude baada ya kupigiwa simu na wakazi wa Inyala ambao baada ya kumuona, walimpeleka katika ofisi ya kijiji hicho na kupatiwa huduma ya kwanza.
Alisema kabla ya kutekwa aliliona gari lenye vioo vyeusi likiwa limeegeshwa kwa muda mrefu nje ya ofisi yake lakini hakuona watu wakishuka wala kupanda kwa kuwa katika ofisi hiyo huweza kuona kila kinachoendelea nje
“Kutokana na matukio ninayokumbana nayo mara kwa mara huwa ninajihami na hurejea nyumbani kabla ya saa 12 jioni. Wakati nikijiandaa kutoka mmoja wa watu katika gari alishuka na kuja ofisini akitaka kununua vocha huku akichezea simu.”
“Nilimjibu siuzi vocha ila mwendo aliotoka nao akirejea kwenye gari ulinishtua nikaamua kuondoka mara moja nikaweka sawa vitu vyangu. Nilipofika mlangoni wakaja watu watatu wakanizunguka wakasema wao ni maaskari, nikawaomba vitambulisho wakahamaki,” alisema Mdude.
Alisema wakati akirudi nyuma kujihami baada ya mmoja wa watu hao kuanza kumsogelea kabla ya hajatupa begi lake lililokuwa na kompyuta mpakato yake katika chumba kimojawapo, mmoja wa watu hao aliwaeleza wenzake kuwa wachukue begi hilo na simu yake kwani ndivyo vya muhimu.
“Mmoja aliniwahi akachukua begi nikaanza kuvutana nao nikipiga kelele kuomba msaada niliamini nitasikika maana kutoka ofisini kwangu na kilipo kituo cha polisi ni kama mita 600 hivi na kuna benki karibu na huwa kuna askari wanalinda.
“Walinifumba mdomo ila nikawa nawang’ata nikitaka sauti yangu ya kuomba msaada isikike. Walininyang’anya vitu vyangu. Pale ofisini nilikuwa na wadogo zangu (wanaofanya kazi ofisini kwake) na watu wengine walisogea karibu ila nje alikuwamo mmoja akiwa na bastola akitisha wasisogee,” alidai Mdude.
Alisema waliokuwa wamesogea karibu waliogopa na kwenda mbali zaidi wakati yeye akipambana na watu hao kabla ya kuzidiwa nguvu na kupakiwa katika gari.
“Katika gari waliendelea kunishambulia huku wakiniziba mdomo. Walinipiga kwa chupa za bia kabla sijapoteza fahamu mmoja nilimsikia akisema tayari wameniua akisema nimevimba sana. Niliwasikia wakisema ‘sisi si wa 2016 sisi tunamaliza kabisa,” alisema Mdude.
Alisema baada ya kupoteza fahamu hakujua kilichoendelea hadi siku ya tano aliposhtuka na kujikuta amelala katika majani na kisha akabaini kuwa alikuwa amefungwa plasta mdomoni na kitambaa usoni, vitu ambavyo aliviondoa na kuanza kutambaa.
“Nilifika barabara kuu ya Mbeya-Tunduma. Nilikaa hapo kwa saa nzima nikinyoosha mkono kuomba msaada. Baadaye alipita bodaboda ambaye awali alinipita na kisha kurudi. Nilimueleza hali yangu nikitaka anipeleke kwa mtu yeyote wa Chadema.”
“Nikamtaka anipeleke polisi kama anaogopa. Nilimuomba pia anipe biskuti na maji ninywe alisema hawezi kunibeba akaondoka na kwenda kumchukua mwenzake ambaye alinitambua vyema akisema aliona picha zangu katika vyombo vya habari.”
Alisema watu hao walimpeleka kwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtakuja ambako walimpa uji na maji ya moto.
Aliwaomba wawatafute viongozi wa Chadema. Mwenyekiti alikuwa na namba ya Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi ambaye alipopigiwa simu alituma watu wakamchukua na kumpeleka hospitali.


Loading...

No comments: