FAMILIA YAMLILIA MWANAFUNZI WA KITANZANIA ALIYEFARIKI MAREKANI - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, May 10, 2019

FAMILIA YAMLILIA MWANAFUNZI WA KITANZANIA ALIYEFARIKI MAREKANI

"Tumepokea taarifa hizi kwa masikitiko makubwa. Alipenda sana masuala ya utabibu, na alienda Marekani kupata mafunzo na kutekeleza ndoto zake," imeeleza familia ya kijana Allen Buberwa, ambaye amefariki nchini Marekani mwanzoni mwa wiki.Buberwa, 22, ambaye alikuwa ni mwanafunzi unesi katika chou cha North Arkansas College alifikwa na umauti baada ya kuteleza na kutumbukia kwenye mto Buffalo. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 12 jioni jimboni Arkansas, Marekani.

Taarifa rasmi zinaeleza kuwa, Buberwa na rafiki zake watatu walienda mtoni huku wawili kati yao wakiingia majini na kuogelea. Buberwa pamoja na kijana mwengine walisalia ukingoni mwa mto.

Ghafla Buberwa aliteleza na kutumbukia mtoni na kushindwa kujinasua, kijana mwenzie aliyekuwa naye pia alijirusha ili amuokoe lakini pia akanasa. Rafiki zao wawili waliotangulia mtoni walijitahidi kuwaokoa lakini Buberwa alisalia chini ya maji.

Vikosi vya uokozi viliupata mwili wake majira ya saa tano usiku wa siku hiyo hiyo ya tukio.

"Kwa ujumla tumeupokea msiba huu kwa masikitiko makubwa sana, na tumeumia sana juu ya Allen," mjomba wa marehemu na msemaji wa familia Bw Philbert Simon ameiambia BBC na kuongeza, "Baba (wa Allen) yupo kwenye hali mbaya, anaumia sana, ndio kijana wake mkubwa, anaumia sana juu ya kijana wake."

Bw Simon anasema Buberwa alipata chuo Marekani baada ya kufanya jitihada binafsi mtandaoni akishirikiana na wazazi wake.

Kwa sasa mwili wa marehemu upo kwenye jumba la kuhifadhia maiti la Coffman Funeral Home of Harrison of Harrison and Jasper, na kwa mijbu wa Bw. Simon, wanaraji mwili huo kuwasili Tanzania kati ya Jumatano au Alhamisi wiki ijayo na mazishi yanarajiwa kuwa siku moja baada ya kufika.

Gharama za kuhifadhi na kusafirisha mwili huo mpaka Tanzania zinakadiriwa kufikia dola 14,000. "Jitihada za kuurejesha nyumbani mwili wa kijana wetu zinaendelea nchini Marekani. Kuna Watanzania wanaoishi kule wanafuatilia suala hili, wanafunzi wenzake pia wanachangishana lakini bado tunahitaji mchango wa kila mtu kutoka kila upande ili kufanikisha kumleta mpendwa wetu.
 

Wasifu wa marehemu

Allen alizaliwa jijini Dar es Salaam, Tanzania Agosti 31, 1996.

Ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne ya Bw Audatus Rwegalulira na Bi Hilda Simon. Ameacha wadogo zake watatu mapacha Christina na Christabella, na wa mwisho Anatolius.

Alianza safari yake ya awali katika shule ya msingi St. Mary's na baadae kuhamishiwa nchini Uganda kwenye shule ya msingi ya Leons Junior hadi darasa la saba.

Aliendelea na masomo ya sekondari Uganda, kidato cha kwanza mpaka cha nne katika shule ya kidato cha kwanza mpaka cha nne St Henry 's College Kitovu na kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari Masaka. Alimaliza safari yake ya elimu Uganda 2016.

"Baada ya hapo alianza harakati za kutafuta chuo, na alipenda sana kupata elimu ya kiwango cha juu sana na jambo jilo ndilo lililomsukuma kuelekea Marekani. Alitamani kufanyakazi kwenye sekta ya afya," amesema mjomba wa marehemu, Bw Simon.
 

Chanzo:BBC SWAHILI

Loading...

No comments: