MWANZA: MWANAFUNZI AJITEKA NA KUDAI FEDHA KWA WAZAZI WAKE - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, May 2, 2019

MWANZA: MWANAFUNZI AJITEKA NA KUDAI FEDHA KWA WAZAZI WAKE


POLISI mkoani Mwanza inamshikilia mwanafunzi wa kidato cha pili anayesoma Shule ya Sekondari St Apostos, Yela Sylvester maarufu Cosmas (17), kwa kosa la kudanganya wazazi wake kuwa ametekwa ili ajipatie fedha.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Jumanne Muliro amewaeleza waandishi wa habari kuwa tukio hilo ni la Aprili 27, mwaka huu saa nne usiku katika Mtaa wa Mahaha wilayani Magu.

Amesema hiyo ni baada ya kijana huyo kusindikizwa kwenda shule na mzazi hadi kwenye Kituo cha Mabasi cha Buzuruga jijini Mwanza na kupakizwa kwenye basi la Sheratoni, linalofanya safari zake kati ya Mwanza na Geita.

Lakini, hakwenda shule na badala yake aliitumia simu namba 0689447247 na kutuma ujumbe mfupi kwa baba yake, huku akiificha laini yake ya zamani ya simu, kwa madai kuwa alikuwa ametekwa kwa lengo la kujipatia fedha.

“Kwenye ujumbe aliomtumia baba yake, alidai kuwa endapo wasipomtumia fedha hizo atapelekwa na watekaji nchini Zambia kufanya kazi, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria,” amesema Kamanda Muliro.

Amesema polisi walifanya ufuatiliaji wa taarifa hizo za kutekwa kwa mwanafunzi huyo na kumtia nguvuni kijana huyo akiwa salama Lamadi wilayani Magu, akiwa na laini ya simu aliyoitumia kumdanganya baba yake kuwa alikuwa ametekwa.

“Tunaendelea kumhoji na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake,” alisema Kamanda Muliro.

Katika tukio jingine, Polisi imewakamata watu watatu kwa kosa la kupatikana na kilogramu 15 za bangi na watuhumiwa wengine wawili kwa kosa la kupatikana na pombe ya moshi lita 33.

Kamanda Muliro alisema tukio hilo ni la kati ya Machi na Aprili katika operesheni kabambe inayoendelea.

Aliwataja watu waliokamatwa na bangi kuwa ni John Marwa (26), Bhoke John (30) na Maria Stephano (25) wote wakiwa ni wakazi wa Kishiri Wilaya ya Nyamagana.

Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa na lita 33 za pombe ya moshi kuwa ni Mkemwa Matono (45), mkazi wa Fumagila na Vedastina Tibikunda (30) ambaye ni mkazi wa Bugarika jijini Mwanza.

“Tunaendelea kuwahoji watuhumiwa, na siku hizi mtaona waliokamatwa ni wanawake, siku hizi unakuta mwanamke anasafirisha bangi kama furushi,” alifafanua. Aliongeza kuwa polisi inaendelea na mahojiano na watuhumiwa watafikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.
Loading...

No comments: