REGINALD MENGI ALIVYOTOKA KUTEMBEA PEKU HADI KUWA TAJIRI MKUBWA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, May 2, 2019

REGINALD MENGI ALIVYOTOKA KUTEMBEA PEKU HADI KUWA TAJIRI MKUBWA

Tanzania imepoteza mmoja wa watu muhimu aliyeacha athari katika maisha ya wengi. Tajiri maarufu nchini, Reginald Mengi aliyefariki usiku wa kuamkia leo Mei 2, 2019 akiwa Dubai.

Reginald Mengi

Ameondoka akiwa amecha urithi wa kitabu ambao pamoja na mambo mengineyo anaelezea wasifu wake ikiwamo safari yake ya maisha ya dhiki akiwa mtoto hadi kuwa msomi mkubwa fani ya uhasibu na kisha tajiri wa kupigiwa mfano.

Wasifu huo aliouita kwa jina la ‘I Can, I Must, I Will, The spirit of success,’ Mengi anaelezea maisha ya kubangaiza waliyokuwa wakiishi wazazi wake katika vibanda vya udongo katika kijiji cha Nkuu kilichopo Machame mkoani Kilimanjaro.

Akiwa mmoja wa watoto saba wa mzee Abraham Mengi na mkewe Ndeekyo, Mengi anasimulia:

“Familia yetu ilikuwa masikini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini. Tulimiliki sio zaidi ya ekari moja tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng’ombe wachache na kuku. Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile.

Hivi ndivyo anavyoanza kusimulia Mengi ambaye ugumu wa maisha tangu utotoni ndio uliomsukuma kaka yake Elitira kuanza kufanya biashara ya kuuza mayai wakati huo akiwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi.

Mbinu za Elitira katika ujasiriamali zikamvutia mdogo wake, ambaye katika kitabu anasema zilimvutia sana. Anasema Elitira alipewa kipawa cha kugundua fursa na kuzigeuza kuwa biashara.

Ni kwa sababu hiyo haikuwa ajabu kwa miaka kadhaa baadaye Mengi naye akaanza kujenga himaya ya biashara baada ya kugundua kuwapo kwa uhaba wa kalamu za wino ambazo miaka ya 1983 ilikuwa ni bidhaa iliyoagizwa kutoka nje.

Huu ukawa mwanzo wa Mengi kuingia katika ulimwengu wa biashara akianza na utengenezaji wa kalamu alizozipa jina la ‘Epica. Anasema alianza biashara hiyo kwa kuagiza vifaa kutoka Mombasa akiwa hana senti mfukoni bali kwa makubaliano ya kulipa baada ya mauzo.

Kutoka kukusanya vifaa vya kutengeneza kalamu, Mengi akazidi kutanua wigo wa biashara kadri siku zilivyokwenda.

Mpaka anaaga dunia, Mengi anatajwa kama mmoja wa matajiri wakubwa nchini na pengine ukanda wa Afrika Mashariki akiwa na himaya ya biashara ya vyombo vya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini.

Mwaka 2014, jarida la Fobes lilimuorodhesha akiwa nafasi ya 45 kati ya matajiri 50 zaidi barani Afrika akiwa na utajiri upatao Dola za Marekani 560 milioni sawa na zaidi ya Sh 1.2 trilioni.

Chanzo: Mwananchi
Loading...

No comments: