MAMBO MANNE YALIYOWAPA TORONTO RAPTORS UBINGWA WA NBA 2019 - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, June 14, 2019

MAMBO MANNE YALIYOWAPA TORONTO RAPTORS UBINGWA WA NBA 2019


Alfajiri ya leo timu ya Toronto Raptors yenye makazi yake nchini Canada imeshinda mchezo wao wa 4 katika mfululizo wa michezo ya fainali za NBA kwa msimu wa 2018/2019 na kuibuka mabingwa wapya wa ligi hiyo pendwa ya kikapu ulimwenguni.

Ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kuchukua ubingwa/kombe hilo na hakika wameweka historia. Zifuatazo ni point chache zilizochangia kwa kiasi kikubwa kwa Toronto Raptors kuchukua ubingwa huku wakiushangaza Ulimwengu uliokuwa umewapa Warriors Ushindi hata kabla ya fainali kuanza:

1. TEAMWORK:
Pamoja na kutokuwa na mastaa wakubwa wengi kwenye timu yao, Raptors wamekuwa wakicheza kwa umoja sana bila kumtegemea mtu mmoja au wawili. Ukiangalia mechi zao nyingi wanazoshinda, mgawanyo wa pointi zao huwa ni mzuri. Hawapishani sana katika kushambulia na hata kuzuia pia. Wanashambulia wote na wanakaba wote.

Raptors
Wachezaji wa Toronto Raptors wakipongezana katika moja ya michezo yao

Muda wote walionyesha kutaka Ubingwa, na kuionyesha dunia kuwa INAWEZEKANA. Walikuwa wana njaa kubwa sana ya mafanikio na kila mmoja alipambana kweli kweli kuhakikisha timu inashinda katika kila mechi zao.

Wamekutana na mengi ya kuwakatisha tamaa na hata kuitwa "under dog" mbele ya wababe wengi lakini wameonyesha kuwa "mpira unadunda" hata kwenye basketball.

2. UBORA WA KAWHI LEONARD:
Hakuna mtu anayebisha kuhusu KAWHI LEONARD kupewa tuzo ya Nba Final MVP kwani ameonyesha kile ambacho watu walitarajia kukiona. Kawhi alijiunga na Raptors mwanzo wa msimu huu akitokea San Antonio Spurs katika dili lililomhusisha DeRozen kwenda Spurs pia.

Toronto Raptors
Mchezaji wa Raptors, Kawhi Leonard akiwa na tuzo yake ya Nba Finals MVP 

Mwisho wa msimu ndio huu na inaonekana kuwa mabadilishano yale ya wachezaji yamewanufaisha zaidi Toronto Raptors ambao leo wametawazwa kuwa mabingwa wapya wa NBA.

Kawhi alikuwa akichangia sana katika ushindi wa timu yake huku akimaliza michezo mingi na point zaidi ya 25 na kuiwezesha kufanya vyema. Na katika mechi ambazo zilikuwa ngumu mno kwao, Kawhi alionyesha uzoefu wake na kuibeba timu hiyo mgongoni.

3. KUKOSEKANA KWA KEVIN DURANT:
Kuumia na kukosekana kwa SNIPER, Kevin Durant wa WARRIORS kumeifanya hii fainali kuwa 50/50. Warriors wakikamilika huwa wanatisha bwana. Asikwambie mtu. Unashindaje kwenye kikosi chenye Stephen Curry, KD, Klay, Draymond na Demarcus Cousin?


Mchezaji wa Golden State Warriors, Kevin Durant akitolewa nje baada ya kuumia

Kwanini KD? Ukiangalia fainali 2 zilizopita ambazo Warriors wamebeba ubingwa, utagundua kuwa KD alikuwa akiwabeba na kuwafanya wawe bora zaidi. Ndio maana alishinda tuzo ya NBA FINAL MVP mara 2 mfululizo katika fainali zote hizo alizoshiriki.

Ubora na uzoefu wake sio wa kutilia shaka na ni mchezaji ambaye huwa anakupa point zaidi ya 35 kwa mchezo mmoja. Hebu patia picha jamaa angekuwepo unadhani mambo yangekuwa hivi? HAPANA. Warriors wangeshinda hii series.

4. KUUMIA KWA KLAY THOMPSON:
Alfajiri ya leo mchezaji wa Warriors, KLAY THOMPSON alikuwa katika mood nzuri mno na alikuwa anatupia vikapu kama hana akili nzuri. Kwa bahati mbaya sana na yeye akaumia goti katika Quarter ya 3 ya mchezo na kufanya timu ibaki na Stephen Curry peke yake kama mchezaji pekee anayeweza kurusha mipira ya mbali/nje ya box.

Klay Thompson
Mchezaji wa Golden State Warriors, KLAY THOMPSON akiugulia maumivu

Kukosekana kwa KD, na kuumia kwa KLAY wakati wakiwa na matumaini ya kushinda mchezo huo, kuliwapa nguvu mpya Raptors ambao walionekana kupambana kweli kweli baada ya kuona gap hilo limetokea.

Mpaka anaumia Klay alikuwa na point 31. Hebu fikiria angebaki. Warriors wangeshinda hii game na tungesubiri mpaka wiki ijayo kupata mshindi.

HONGERA KWA RAPTORS:
Mwisho kabisa nitoe pongezi kwa timu ya Toronto Raptors kwa kushinda taji hili katika mazingira ambayo hakuna mtu aliyewapa nafasi. Wamanatuonyesha kuwa ukiwa na nia, ukapambana, basi mafanikio yanakuja tu.

Toronto Raptors
Mabingwa wa NBA 2018/2019 Toronto Raptors


Loading...

No comments: