Mazishi ya Bibi Harusi na Wenzake, Vilio Vyatawala

Vilio na simanzi vimetawala nyumbani kwa familia ya Jackson Mwandunga wilayani hapa Mkoa wa Mbeya baada ya kuwasili miili minne ya familia hiyo akiwamo aliyekuwa bibi harusi mtarajiwa, Diana Mwandunga.

Miili hiyo imewasili leo Ijumaa asubuhi Juni 21, 2019 ikitokea Hospitali ya Rufaa Mbeya ilikokuwa imehifadhiwa baada ya watu hao kufariki dunia kwenye ajali ya gari ndogo juzi Jumatano eneo la Machimbo barabara kuu ya Mbeya-Makambako.

Wengine waliofariki dunia kwenye ajali hiyo ni Faraja Mwandunga, James Mwandunga na mtoto wa Faraja, Jacton (2) wakati waliojeruhiwa ni Ibrahimu Mwandunga na Nico Mwandunga.

Ajali hiyo ilitokea baada ya ndugu wa familia hiyo, kumuaga ‘Send off’ Diana katika sherehe iliyofanyika Jumamosi iliyopita ya Juni 16 nyumbani kwao Chimala, Mbarali na Juni 26, 2019 ilitarajiwa kufanyika Send Off nyingine jijini Dar es Salaam kisha ndoa Juni 29, 2019.

Vilio vimetawala baada ya majeneza yaliyobeba miili ya ndugu hao ilipowasili nyumbani kwa ajili ya maziko yatakayofanyika leo Ijumaa.

Miongoni mwa wahudhuriaji wa mazishi hayo ni bwana harusi Elisante Edward ambaye mara zote anaonekana kutokwa machozi huku akisaidiwa na ndugu kumfariji.

Kutokana idadi kubwa ya waombolezaji waliojitokeza, shughuli ya kuaga miili hiyo imehamishiwa  uwanja wa mpira wa stendi mpya Chimala.

Post a Comment

0 Comments