TAIFA STARS WAPAMBANA LAKINI JUHUDI ZAO HAZIKUTOSHA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, June 28, 2019

TAIFA STARS WAPAMBANA LAKINI JUHUDI ZAO HAZIKUTOSHA

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars jana usiku ilikuwa uwanjani katika michuano ya mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON 2019 dhidi ya majirani zetu wa Kenya Harambee Stars katika mechi ya pili katika kundi C ambalo wapo. 

Kapteni wa Taifa Stars
Kapteni wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akishangilia goli alilofunga hapo jana dhidi ya Kenya
Mechi hiyo iliyoisha kwa Taifa Stars kupoteza mchezo kwa mabao 3-2 licha ya kuwa mbele muda mrefu, ilikuwa ya kuvutia sana kwa pande zote mbili huku kila timu ikiiangalia mechi hiyo kama mkombozi kwani kila moja ilikuwa imepoteza mechi ya kwanza na hakuna matumaini ya kushinda mechi ya mwisho ya makundi. 

Kipindi cha kwanza kiliisha kwa Taifa Stars kuongoza kwa magoli 2-1 huku magoli ya Stars yakifungwa na Simon Msuva dakika ya 6 na kapteni Mbwana Samatta dakika ya 40. Goli la Kenya lilifungwa na Michael Olunga dakika ya 39. 

Kipindi cha pili mambo yakabadilika bwana. Wakenya walionyesha kutaka kupindua matokeo na waliona kabisa kuwa inawezekana. Magoli mawili ya Omolo na Michael Olunga tena yalitosha kabisa kuwapa ushindi Harambee Stars ambao wanajihakikishia nafasi ya 3 katika kundi C na wanahitaji kumfunga Senegal tu ili kujihakikishia kusonga mbele katika hatua ya 16 bora. 

Mipira ya kutengwa imebaki kuwa tatizo kwa Taifa Stars yenye mabeki wafupi na kipa asiyejua kuitolea mbali mipira hiyo. Magoli mawili ya wakenya yametokana na mpira wa kona na faulo. 

Kenya Vs Tanzania
Wachezaji wa Harambee Stars (Kenya) wakishangilia moja ya magoli yao dhidi ya Taifa Stars hapo jana

Kiuchezaji, timu yetu ilionyesha mpira mzuri zaidi jana kuliko mechi ya kwanza dhidi ya Senegal. Jana Taifa Stars walipiga mashuti 11 huku 5 yakilenga lango wakati mechi ya kwanza dhidi ya Senegal tulipiga mashuti 3 tu na hakuna hata moja lililolenga lango. Uhakika wa pasi ulikuwa ni 70% na tulipiga pasi 285. 

Vijana wetu wamepambana sana jana lakini juhudi zao hazikutosha kutuhakikishia ushindi. Bado tuna mechi moja ya mwisho ya makundi dhidi ya Algeria. 

Loading...

No comments: