UFARANSA NA UJERUMANI ZAKUMBWA NA JOTO KALI


Nchi za Ulaya kaskazini zimekumbwa na joto kali lisilokuwa na kifani mnamo wiki hii. Mamlaka husika nchini Ujerumani na Ufaransa zimejiweka katika hali ya tahadhari.

Watalaamu wa mambo ya hali ya hewa wamesema, kuongozeka kwa viwango vya joto duniani ni ushahidi mwingine wa kuendelea kwa mabadiliko ya tabia nchi. Idara kuu ya hali ya hewa imesema kiwango cha joto leo kinatarajiwa kufikia nyuzi joto 38 hapa nchini Ujerumani.

Mtaalamu wa mambo ya hali ya hewa Sabine Krueger amesema viwango vya joto vinaweza kuvunja rekodi hadi kufikia nyuzi joto 40 kwenye baadhi ya maeneo ya Ujerumani kama vile sehemu zinazouzunguzka mji maarufu wa Frankfurt ulioko kwenye jimbo la kati la Hesse.
Mnamo mwaka 2015 sehemu za jimbo la kaskazini, Bavaria zilifikia nyuzi joto 40.3. 

Hata hivyo mtaalamu huyo wa hali ya hewa Sabine Krueger amesema baadhi ya maeneo yatafikia nyuzi joto 29 tu hasa kwenye ukanda wa bahari ya kaskazini. Madaktari wana wasiwasi juu ya viwango hivyo vya joto.

Watu wakijipumzisha kwenye madimbwi ya maji kutokana na jioto kali
Daktari wa kitengo cha dharura kwenye hospitali ya mjini Berlin Simon Trach ameeleza kwamba makundi mawili ya watu ndiyo hasa yanayoweza kukumbwa na matatizo ya afya kutokana na joto kali. Kwanza kabisa ni watoto. 

Amesema watoto chini ya umri wa miaka 2 wanashauriwa kutojianika juani kwa sababu ya hatari kubwa ya kupata maradhi ya saratani ya ngozi katika maisha yao ya baadae. 

Kundi jingine ni la wazee wenye matatizo ya afya kama vile ya figo na moyo na kukaukiwa maji mwilini. Ikiwa hawanywi maji ya kutosha wakati wa joto kali wanaweza kupata matatizo makubwa zaidi.

Wataalamu wa hali ya hewa wametahadharisha kwamba zaidi ya nusu ya Ufaransa inaweza kufikia kiwango cha nyuzi joto 40. 

Idara kuu ya utabiri wa hali ya hewa nchini Ufaransa imetoa tahadhari ya kiwango cha juu kabisa ya kuwataka watu wawe waangalifu sana, hasa wakati ambapo msimu wa watalii umepamba moto nchini humo.

Mashirika ya misaada yamepeleka wahudumu mitaani katika mji mkuu Paris ili kuwahudumia watu waisokuwa na makaazi, na idara ya serikali za mitaa zimetenga sehemu maalumu zilizowekea vipunga hewa na viyoyozi. Kutokana na joto kali mitihani ya watoto wa shule imeahirishwa hadi wiki ijayo.

Shirikisho la kandanda duniani,FIFA pia litapaswa kutilia maanni hali hiyo ya joto kali wakati ambapo mashindano ya kombe la dunia ya wanawake yanafanyika nchini humo. 

Yumkini itapasa kubadilisha ratiba ya mashindano. Ufaransa bado inawakumbuka watu zaidi ya15,000 waliokufa kutokana na joto kali mnamo mwaka 2003.


Post a Comment

0 Comments