BERNARD MEMBE AKIRI SAUTI ILIYOSAMBAA AKIONGEA NA SIMU NI YAKE - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, July 30, 2019

BERNARD MEMBE AKIRI SAUTI ILIYOSAMBAA AKIONGEA NA SIMU NI YAKE

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amezungumza kuhusu mawasiliano yake ya simu kudukuliwa, huku akikiri sauti iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hivi karibuni ni yake.Katika mahojiano na moja ya vituo vya redio jijini Dar es Salaam jana, Membe alikiri mawasiliano yake kudukuliwa na kutoa tahadhari kwa kampuni za mawasiliano ya simu kwa kuwa changamoto hiyo huenda ikazitia hasara kubwa.

"Sauti ni za kwangu, ni mimi 100 kwa 100 na nimeifanyia kazi na ninajua imetoka wapi kwa sababu nina miiko ya kuzingatia sisemi.

"Ni sauti ya kwangu kabisa na ninaelewa kila kilichotokea. Unaweza kuingia ugonjwa wa udukuzi, kama wale wanaotoa taarifa hizi za udukuzi hawachukuliwi hatua, 'hackers' (wadukuzi) wapo duniani, wanataka fedha tu.

"Ni kosa la jinai kudukua mawasiliano ndiyo maana dunia nzima huwasikii wanadukuana waziwazi. Hapa kwetu watu wenye wajibu wa kukataza udukuzi ni TCRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano) mitandao yote ipo chini yao.

"Tuna sheria zipo, sheria mpya ya mwaka 2013, sidhani kama imerekebishwa, inakataza katakata udukuzi na dunia nzima hamuisikii ikifanya hayo kwa sababu mbili kubwa:

"Sababu ya kwanza, ukidukua yule anayedukuliwa akalalamika, utapata adhabu kubwa sana ndiyo maana dunia haigusi eneo hili, wanadukua na vyombo vya usalama wanadukua lakini haviwezi kutoa 'public' (waziwazi) 'information' (taarifa) ambazo ni 'top security' (usalama wa hali ya juu).

"Lakini, kuna baya zaidi ya hili nililolisema, kama hilo moja halitoshi, sikiliza hili la pili kwa umakini, sababu ya pili inayofanya dunia isitake kutoa taarifa za udukuzi nje nchini ni kwamba hii ni biashara.

"Mimi Membe leo nikiona nimedukuliwa na mtu mwingine yeyote yule, siyo lazima niende kwenye chombo cha sheria nikalalamike kudai fidia, hata kidogo. Dunia itakapojua wajanja, wataalamu wa IT na 'hackers' (wadukuzi) wataingia jijini Dar es Salaam."Alipotafutwa na kituo hicho cha redio kuzungumzia suala hilo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema serikali imeandaa muswada ili kutunga sheria kulinda taarifa za mtu binafsi kudukuliwa.

"Udukuzi upo mkubwa tu, ni suala la teknolojia, vijana kwenye IT wanatengeneza mawazo mengi kwa siku, kwa hiyo wanafanya majaribio mengi.

"Nikupe mfano mmoja, ATCL (Shirika la Ndege) wakati tunaanza tulidukuliwa kwenye ukataji wa tiketi, bahati nzuri aliyekuwa anatudukua ni bwana mdogo aliyekuwa anaifanya hiyo kazi, amesoma IT (teknolojia ya habari) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

"Tukamtafuta na kumkamata, kwa hiyo udukuzi si kwamba upo Tanzania tu, hata duniani upo, siyo sisi tu huku," alisema.

Siku chache baada ya makatibu wakuu wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba kutoa waraka wakilalama kudhalilishwa na mtu anayejiita mwanaharakati huru, mawasiliano ya simu yenye sauti zinazodaiwa zao, yalisambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Baadaye mawasiliano ya simu ya Membe yalisambazwa kwenye mitandao hiyo.

No comments: