MBARONI KWA KUMCHINJA MKEWE HANDENI, TANGAJuma Hemedi (45) mkazi wa mtaa wa Kwamaraho kata ya Malezi wilayani handeni, anashikiliwa na polisi akituhumiwa kumuua mkewe Amina Husein (38) kwa kumchinja shingo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Edward Bukombe amethibitisha kutokea tukio hilo na kusema lilitokea usiku wa kuamkia Julai 8 huku chanzo chake ni sababu za kimapenzi ambapo kulikuwa na ugomvi wa kifamilia na polisi wanafuatilia kwa undani zaidi.

"Taarifa za awali zinasema sababu za mauaji hayo ni za kimapenzi, kwamba marehemu na mumewe walikuwa na mgogoro wa kifamilia na sisi kama polisi tunafuatilia kwa undani zaidi ili kupata undani wa tukio hilo," alisema Bukombe.

Diwani kata ya Malezi, Shabani Kitombo akiwa eneo la tukio amelaani kitendo hicho na kusema kuwa inaonyesha mwanamke huyo amekatwa panga eneo la shingoni.

Alisema kitendo hicho ni cha kinyama na haijawahi kutokea hapo kabla katika uongozi wake kwa mwananchi kuuawa kinyama kiasi hicho kwa kuchinjwa shingo.

Jophrey Kisanga, ambaye ni mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu alisema wamekuta una jeraha la kukatwa na panga katika upande wa kushoto wa shingo yake.

Post a Comment

0 Comments