POLISI KUCHUNGUZA SAUTI ZINAZODAIWA KUWA ZA VIONGOZI

Wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikisema sauti zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikihusisha sauti zinazofanana na baadhi ya makada wa CCM ni tukio la jinai, polisi wanaendelea na uchunguzi.Sauti hizo fupi za mazungumzo ya simu zinadaiwa kuwa za Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye; aliyekuwa waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba; makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba pamoja na waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Benard Membe.

Akizungumza na Mwananchi jana, msemaji wa TCRA, Semu Mwakyanjala alisema kwamba hiyo ni jinai na wenye mamlaka ya kuchunguza jinai ni Jeshi la Polisi.

Mwananchi lilitaka TCRA wazungumzie mawasiliano ya simu ya wananchi yako salama kwa kiwango gani.

“Hii ni jinai na mwenye mamlaka kuchunguza ni polisi, sisi tutawapa ushirikiano wakihitaji na tumekuwa tukifanya hivyo kila wanapohitaji,” alisema.

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alisema bado wanachunguza ili kubaini ukweli. “Hakuna jambo kama hilo linaweza kupita tusilichunguze.”


SOURCE: MWANANCHI

Post a Comment

0 Comments