Vodacom yazindua M-Pesa Songesha, huduma mpya inayokuwezesha kutumia pesa zaidi ya kiwango ulichonacho - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, July 11, 2019

Vodacom yazindua M-Pesa Songesha, huduma mpya inayokuwezesha kutumia pesa zaidi ya kiwango ulichonacho

Mkurugenzi wa 'M-Commerce' Vodacom Tanzania (Wapili kushoto), Epimarck Mbeteni , Mkuu wa kitengo cha huduma kwa wateja Bi.Herieth Lwakatare (watatu kulia) na  Mkurugenzi wa Wateja wa Mikataba (Business Enterprise Unit), Arjun Dhillon (wa kwanza kulia) wakishikana mikono na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Hatari na Utekelezaji, Moses Manyatta (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Masoko na Maendeleo ya Biashara, Deogratius Kwiyukwa (watatu kushoto) na Mkuu wa matawi, Bonaventura Paul (wapili kulia) kutoka Tanzania Postal Bank (TPB) , kuashiria uzinduzi wa huduma mpya ya kifedha iitwayo 'M-Pesa songesha' amabayo inawawezesha wateja wa Vodacom Tanzania kutumia fedha zaidi ya kiwango walichonacho kwenye akaunti zao, Dar es Salaam, Jana.  Kampuni ya Vodacom imedhamiria kubadili Tanzania kuwa jamii inayofanya malipo kidigitali zaidi.

 Mkurugenzi wa 'M-Commerce' Vodacom Tanzania, Epimarck Mbeteni akizungumza katika sherehe ya uzinduzi wa huduma mpya ya kifedha itwayo 'M-Pesa songesha' amabayo inawawezesha wateja wa Vodacom Tanzania kutumia fedha zaidi ya kiwango walichonacho kwenye akaunti zao, Dar es Salaam, jana. Kampuni ya Vodacom imedhamiria kubadili Tanzania kuwa jamii inayofanya malipo kidigitali zaidi.

9th Julai 2019, Dar es Salaam – Kampuni inayoongoza nchini kwa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao wa simu, Vodacom, leo imezindua huduma ya kwanza na ya kipekee nchini ambayo inaruhusu wateja wa M-PESA kukamilisha miamala wakati hawana fedha za kutosha katika akaunti zao za M-PESA. Uvumbuzi huu wa kibunifu uitwao M-Pesa Songesha umezinduliwa leo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya kampuni hiyo.
Kwa kutumia huduma hii, wateja wa M-Pesa sasa wataweza kutumia huduma hii kwa urahisi zaidi wakiwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukamilisha miamala yao kama vile kulipia bili, kutuma pesa kwa ndugu jamaa na marafiki au hata kununua bidhaa pasipo kuwa na fedha za kutosha katika akaunti zao.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi wa M-Commerce, Epimack Mbeteni alisema, "dhamira yetu ya kuleta mifumo bunifu ya kifedha kwa kutumia simu za mkononi ilitupelekea kutazama kwa makini vikwazo vya mara kwa mara vinavyowazuia wateja wetu kukamilisha miamala yao kwa sababu ya upungufu wa fedha katika akaunti zao. Uchunguzi huo umepelekea kuja na ufumbuzi wa kibunifu wa wateja wetu kuweza kukamilisha miamala ya M-Pesa ambayo ingeshindikana kukamilika kwa sababu ya upungufu wa fedha".
Songesha ni moja kati ya huduma nyingi za M-Commerce zilizozinduliwa mwaka huu. Huduma hizi ambazo nyingi zinaendana na maisha ya kidijitali zimewezesha Vodacom kuendelea kuongoza katika huduma za simu na fedha nchini kupitia miamala ya simu, umiliki wa soko na wateja. Katika mwaka wa fedha uliomalizika mwezi Machi mwaka huu, M-Pesa iliongeza umiliki wa soko hadi kufikia asilimia 40 na kuingiza watumiaji zaidi ya milioni 9 katika mifumo rasmi ya kifedha ambao wanafanya miamala ya zaidi ya trilioni 4.1 kwa mwezi. 
Watumiaji wa M-Pesa wanaweza kufikia Songesha kwa kupiga namba za huduma ya M-Pesa, *150*00#, kisha kuchagua huduma za kifedha na kujiunga na huduma hiyo ya M-Pesa Songesha. Mara tu baada ya mteja kujiunga na Songesha, atapata ujumbe wa kiwango ambacho anastahili na ataweza kutumia kiwango hicho kukamilisha miamala yake. Kiasi hicho kitarejeshwa pale ambapo mteja atapokea fedha katika akaunti yake ya M-Pesa.
"kiwango hicho kina riba ya asilimia 1 kwa siku 18 na wateja wetu wanaweza kufanya miamala kwa kutumia huduma hii kadri watakavyo ikiwa ni ndani ya kikomo cha kiwango chao. Tumeungana na benki ya TPB kuwezesha huduma hii na ili kuamua kiwango mteja anachostahili, benki itatumia taratibu zilizowekwa kulingana na miamala ya mteja husika katika matumizi yake ya M-Pesa" alisema Epimack.
Akiongea kuhusu huduma hii mpya, kaimu Afisa mtendaji mkuu wa TPB Bank Moses Manyatta alisema, “lengo letu kama benki ni kuhamasisha huduma jumuishi za kifedha huku tukiwahamasisha Watanzania kujenga tabia ya kujiwekea akiba na kujipatia mikopo kwa urahisi, Songesha ni kila kitu na inapatikana masaa 24 kwa siku saba kupitia simu yako ya mkononi! Tunajivunia kuwa na uhusiano huu na tuna Imani kwamba mapinduzi haya yatasaidia katika huduma jumuishi za kifedha,” alisema.
"Tunaendeleza nia ya kubadili Tanzania kuwa jamii inayofanya malipo kidijitali, tunawekeza katika teknolojia ya simu ambayo itaingiza watu wengi zaidi katika mifumo ya kifedha na hatimaye, kufikia malengo ya kijamii na kiuchumi ya nchi." alielezea Mbeteni.

Mwisho

Loading...

No comments: