KUCHANGIA JITIHADA ZA UTUNZAJI MAZINGIRA, SBL YAPANDA MITI 1000 KILIMANJARO

Kama hatua ya kuchangia katika jitihada za utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji mkoani Kilimanjaro, kampuni ya bia ya Serengeti, Serengeti Breweries Limited (SBL) kwa kushirikiana na taasisi ya The Kilimanjaro Project imezindua kampeni ya kupanda miti elfu moja mkoani humo. 

Mjumbe kutoka ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania akishiriki zoezi la upandaji miti lililondaliwa na kampuni ya Serengeti Breweries Ltd mkoani Kilimanjaro

Miti hiyo imepandwa katika kiwanda cha SBL kilichopo Pasua katika wilaya ya Moshi na mingine imepandwa katika wilaya ya Mwanga. 

Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti, amesema SBL imeamua kuongeza jitihada za uhifadhi wa mazingira si tu katika maeneo yaliyo chini ya SBL bali katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. 

“Huu ni udhihirisho tosha kwamba SBL imejidhatiti na iko tayari kushirikiana na wadau wengine katika kutekeleza miradi yenye kuleta tija kwa jamii zetu,” amesema Ocitti. 

Zoezi la upandaji miti linakuja huku kukiwa na wito kutoka jumuiya ya kimataifa juu kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kuongeza juhudi za uhifadhi wa misitu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na hivyo kuyaweka mazingira katika hali ya usalama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.  

Mpango huu wa SBL unaenda sambamba na sera ya kampuni katika kurudisha kwa jamii sehemu ya faida, na umejikita zaidi katika utoaji wa huduma bora ya maji safi kupitia mradi uitwao Water of Life (WOL); mpango kwa ajili kuwasaidia wanafunzi kupata ufadhili wa masomo ya elimu ya juu, kuwasaidia wakulima wa ndani hususani wa vijijini pamoja na mpango wa kuhamasisha unywaji pombe kistaarabu. 

Zoezi la upandaji miti limehudhuriwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sara Cooke pamoja na Mwakilishi wa Waziri Mkuu wa Uingereza kitengo cha biashara, Andrew Rosindell, ambao walikuwa ziarani kiwandani hapo.  

Post a Comment

0 Comments