WAZIRI SIMBACHAWENE ABAINI KUENDELEA KUTUMIKA KWA MIFUKO YA PLASTIKI KATIKA SOKO LA KARIAKOO

Wafanyabiashara wa soko dogo la Kariakoo, Dar es Salaam nchini Tanzania wanaojihusisha usambazaji na uuzaji wa mifuko ya plastiki laini yenye rangi nyeupe inayotumika kama kifungashio wamepewa siku 14 kuiondoa sokoni mifuko hiyo.Kauli hiyo imetolewa jana Alhamisi Agosti 15, 2019 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) George Simbachawene baada ya kufanya ziara katika soko hilo na kubaini uwepo wa mifuko hiyo kinyume cha utaratibu.

Katika ziara hiyo, Simbachawene aliambatana na maofisa wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), alijionea namna mifuko hiyo iliyopigwa marufuku ikitumika kama kifungashio cha bidhaa za nyanya, karoti, vitunguu ambavyo vinaweza vikabebwa kwenye mifuko mbadala.

Juni Mosi 2019, katazo la marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki lilianza kutumika rasmi, hata hivyo bado kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wamiliki wa viwanda vya plastiki kuendelea kutengeneza mifuko hiyo kinyume cha utaratibu.

Amewaambia wafanyabiashara wanaotumia elimu imeshawafikia lakini kitendo cha wao kuendelea kuiuza mifuko hiyo, kinawapa morali wazalishaji kuendelea na shughuli hiyo kinyume cha sheria.

“Kwani mmelazimishwa kununua mifuko hii kiwandani, kwa nini msichukue mifuko mbadala na kuiuza? Kuna vikapu, mifuko ya karatasi kwa nini msichukue hiyo,” anahoji Simbachawene

“Watumiaji elimu imeshawafikia lakini nyie bado mnaendelea kuiuza. Kitendo cha mifuko hii kuendelea kuwepo sokoni kinawavunja moyo watengenezaji na wazalishaji wa mifuko mbadala.”

Simbachawene alisema taarifa alizonazo kuna viwanda vinne vya plastiki vinajishughulisha na uzalishaji wa mifuko hiyo laini iliyopigwa marufuku na Serikali huku akiwaagiza NENC kuvifuatilia kuanzia kesho.

Mjumbe wa bodi ya wafanyabiashara wadogo wa soko hilo, Rajabu Ally anadai wao hawana kosa bali wenye matatizo ni wenye viwanda vinavyozalisha mifuko hiyo.

Post a Comment

0 Comments