DISEMBA MOSI NI SIKU YA UKIMWI DUNIA, FAHAMU HISTORIA NA LENGO LA SIKU HII.


Disemba 1 kila mwaka Dunia inaadhimisha siku ya Ukimwi. Ni siku inayotumiwa zaidi kutolewa elimu kuhusu namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi, kupiga vita unyanyapaa na kuhimiza watu kwenda kupima na kufahamu afya zao.

Shirika la afya Duniani WHO mwaka 2018 lilitoa taarifa kuwa watu Milioni 37 duniani, wanaishi na maambukizi ya ukimwi huku vijana wakiendelea kuwa hatarini zaidi kuambukizwa hasa barani Afrika.

Watu wengine Milioni 22 walioambukizwa, wanatumia dawa ya AVR ambayo imesaidia watu wengi sana kuendelea kuishi.

Maadhimisho haya yamekuwa yakiadhimishwa tangu mwaka 1988, lengo kubwa likiwa ni kutoa elimu kuhusu namna ya kuepuka ugonjwa huu. Woga, unyanyapaa na kupuuza ni mambo ambayo yanaendelea kuitesa dunia katika mapambano ya ugonjwa huu ambao umesababisha vifo vya Mamilioni ya watu tangu miaka 1980.

Maambukizi mapya yanawaathiri idadi kubwa ya vijana walio na umri wa kati ya miaka 15-25. Uchunguzi wa WHO mwaka jana  ulibaini kuwa, asilimia 71 ya maambukizi mapya yanatokea barani Afrika, hasa eneo la Afrika Mashariki na Kusini.

HISTORIA
Siku ya Ukimwi Duniani ilibuniwa mnamo Agosti 1987 na James W. Bunn na Thomas Netter, maafisa wawili wa habari kwa umma kwa ajili ya Mpango wa Kimataifa juu ya UKIMWI katika Shirika la Afya Duniani mjini Geneva , Uswisi.

Bunn na Netter walichukua wazo lao kwa Dokta Jonathan Mann, Mkurugenzi wa Mpango wa Kimataifa juu ya UKIMWI.

Dr Mann alipenda wazo lao, akaliridhia na kukubaliana na pendekezo kuwa adhimisho la kwanza la Siku ya Ukimwi Duniani iwe tarehe 1 Desemba 1988.

Bunn alipendekeza tarehe hiyo ili kuhakikisha uangalifu wa vyombo vya habari vya Ulaya , kitu ambacho aliamini kuwa muhimu kwa mafanikio ya Siku ya Ukimwi Duniani.

Aliamini hivyo kwa sababu 1988 ulikuwa mwaka wa uchaguzi huko Marekani na vyombo vya habari vingekuwa vimechoka kurekodi habari za uchaguzi na wangekuwa na hamu ya kupata habari mpya.

Bunn na Netter waliona kuwa 1 Desemba ilikuwa muda wa kutosha baada ya uchaguzi na mapema kabla ya likizo ya
Krismasi na hakukuwa na habari kamilifu siku hiyo kwa hivyo ingekuwa siku barabara kuadhimishia Siku ya Ukimwi Duniani.

Post a Comment

0 Comments